TANGAZO
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe ametangaza rasmi nia yake ya kuwania Urais wa Tanzania katika Uchaguzi
Mkuu ujao.
Hata hivyo, akizungumza katika kipindi cha Nyumba ya
Jirani kinachorushwa na televisheni ya taifa, TBC I juzi usiku, Membe alisema
ataanika kila kitu akiwa kijijini kwao Rondo, Lindi Vijijini mkoani Lindi.
“Nitatangaza nia yangu kijijini kwetu nilikozaliwa.
Kule ambako nilianza kupata mwanga wa elimu niliyonayo. “Kule nilikotokea hadi
kwenda Usalama wa Taifa, kule nilikotokea na kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa. Hata safari nyingine (ya kuwania Urais), ni vyema
ikawa na baraka za wazee kule ninakotoka, ndiyo maana nasema nakwenda
kutangazia nia kijijini kwetu.”
Membe ni mmoja wa makada mashuhuri wanaotajwa kuwania
Urais kwa tiketi ya CCM.
Wengine wanaotajwatajwa ni Waziri Mkuu wa sasa,
Mizengo Pinda, mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa,
Steven Wassira, Lazaro Nyalandu, Profesa Mark Mwandosya na January Makamba
waliomo katika Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete na William Ngeleja, aliyewahi
kuwa waziri katika serikali ya Kikwete na Dk Hamisi Kigwangallah, Mbunge wa
Jimbo la Nzega.
Asili ya Membe Alizaliwa Novemba 9, 1953 katika kijiji
cha Rondo Chiponda, wilaya ya Lindi Vijijini, akiwa ni mtoto wa pili katika
familia ya watoto saba wa mzee Camillius Anton Ntanchile na mama Cecilia John
Membe.
Membe alifunga ndoa ya Kikristo na Dorcas Richard
Masanche mwaka 1986 na Mungu amewajalia watoto watatu, wawili wa kiume na mmoja
wa kike.
Kimaisha Membe hakukulia mjini, alizaliwa na kukua
akiwa kijijini kama Watanzania wengi waliokulia huko walivyo, hivyo anajua tabu
wanayopata wanavijiji kwa sababu alizaliwa katika kijiji ambacho hakikuwa na
zahanati na maji yalikuwa shida, alilazimika kutembea kilometa nyingi
kuyafuata.
Kwa upande wa elimu, kwa kiasi kikubwa, Membe amefuata
mtiririko wa kawaida katika kusoma kwake, elimu ya msingi aliipata katika shule
ya msingi Rondo Chiponda mwaka 1962 hadi 1968.
Shule ya sekondari alisomea katika Seminari ya Namupa
(1969 hadi 1972), akajiunga na Itaga Seminari Tabora kwa kidato cha tano na
sita (1973 hadi 1974.) Baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka 1974, Membe
alijiunga kwa mujibu wa sheria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa
mwaka mmoja.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1981/82),
alisomea Shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma akitokea Ofisi ya Rais
alipokuwa ameajiriwa.
Matokeo mazuri chuoni hapo yalimpa nafasi ya kuwa
Mhadhiri Msaidizi, lakini mwajiri wake alimzuia na baadaye alijiunga na Chuo
Kikuu cha Johns Hopkins nchini Marekani mwaka 1992 kwa masomo ya Shahada ya
Uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa.
Mbali ya kufanya kazi katika Idara ya Usalama wa Taifa
tangu mwishoni mwa miaka ya 1970, amekuwa Ofisa wa Ubalozi nchini Canada,
amekuwa pia Waziri wa Mambo ya Nje tangu mwaka 2007, hivyo kumfanya kuwa na
uzoefu mkubwa wa masuala ya kimataifa.
Akiwa Mbunge Jimbo la Mtama kwa miaka 15, amewahi pia
kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na pia Naibu Waziri wa Nishati na Madini
kwa takribani mwaka mmoja kabla ya kuhamishiwa rasmi Mambo ya Nje.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD