TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi
SERIKALI imeshauriwa kutekeleza
kwa vitendo sheria na sera zilizopo katika kupambana na tatizo la mimba za
utotoni nchini pamoja na maambukizi ya VVU(UKIMWI) kwa vijana ili kupunguza
tatizo la mimba za umri mdogo na maambukizi mapya ya Ukimwi kwa kundi hilo
jambo ambalo linapelekea vijana wengi kushindwa kutimiza malengo yao waliojiwekea.
Hayo yalisemwa jana na
vijana mbalimbali wanaotoka katika klabu za vijana zinazojishughulisha na
utoaji elimu kwa vijana wilayani Masasi mkoani hapa kwenye jukwaa la vijana
lililoandaliwa na Mtandao wa maendeleo ya vijana wilayani Masasi(MASAYODEN)
chini ya ufadhili wa mashirika ya DSW, EVERPLAN na GIZ na kufanyika mjini hapa.
Wakizungumza kwa
kuchangia mada ya nini kifanyike juu ya utatuzi wa tatizo la mimba za utotoni
na maambukizi ya Ukimwi kwa vijana,Rerginerda Frank ,Hope Selemani,na Juma
Kabisa walisema Serikali inatakiwa
kutekeleza kwa vitendo sheria na sera zinazolinda na kutoa adhabu dhidi ya watu
wanaowapa mimba wasichana walio na umri mdogo ili iwe fundisho kwa watu wengine
wanaofanya vitendo hivyo kwa kundi hilo.
Walisema changamoto ni
nyingi kwa vijana zinazopelekea kujiingiza katika vitendo vya ngono zembe
wakati wakiwa na umri mdogo na kwamba baadhi ya changamoto hizo ni umasikini wa
kipato kwenye familia zao ikiwa ni pamoja na malezi finyu kwa wazazi na walezi
wanaoishi nao.
Vjana hao walieleza kuwa
ukosefu wa fursa za ajira kwa kundi hilo pia ni chanzo cha mimba za utotoni na
kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa ongezeko
la watoto wa mitaani hivyo serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yashirikiane
katika kusimamia sheria na sera za kumlinda kijana na kumsaidia kuondokana na
changamoto anazokabilianazo.
Nae Faraji Mbaraka na
Alafa Rashidi kutoka klabu ya vijana ya Joging Klabu Masasi walisema ukosefu wa
elimu kwa jamii na kundi la vijana kwa ujumla kuhusu athari za kufanya ngono
uzembe katika umri mdogo ni chanzo moja wapo cha mimba za utotoni na maambikizi
ya VVU kwa vijana.
“Tatizo la serikali
kushindwa kutoa fursa za ajira kwa vijana inapelekea kundi hilo kukosa cha
kufanya katika kujiingizia kipato hivyo tunaamua kujiingiza katika mambo ya
ngono na kupata mimba za utotoni na hata maambukizi ya Ukimwi…tunaomba serikali
na mashirika mtuangalie sisi vijana,”alisema kijana mwingine aliyejitambulisha
kwa jina la Sefu Idrisa.
Walisema elimu ya afya
ya uzazi na jinsia pia inatakiwa kutolewa kwa vijana ili kulifanya kundi hilo
kuwa na uwelewa wa kutosha katika kujilinda na vishawishi vinavyowafanya
wajiingize katika masuala ya ngono wakiwa na umri mdogo elimu ambayo pia
wataitumia kuwapa vijana wengine ambao hawapo kwenye klabu za vijana.
Kwa upande wake katibu
wa Mtandao wa maendeleo ya vijana Masasi (MASAYODEN) Salumu Katondo alisema
kuwa taarifa ya viashiria vya kuongezeka kwa maambukizi ya Ukimwi na mimba za
umri mdogo ilitolewa na TACAIDS taifa hivi karibuni ambako ilieleza kuwa wilaya
ya Mtwara pamoja na Masasi zinaongoza kwa matatizo hayo.
Katondo alisema Mtandao
huo wa vijana wilayani Masasi utahakikisha unawapa elimu ya kutosha kundi hilo
ili liweze kujitambua kiafya,kielimu na kiuchumi na kwamba hatua ya kwanza ni
kupitia mradi huo wa elimu ya afya ya uzazi na jinsia kwa vijana wenye umri wa
miaka 14 hadi kufikia 24 na kuhamasisha kuunda klabu za vijana ili zishirikiane
kupeana elimu mbalimbali waweze kubadili tabia zao.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD