TANGAZO
Dar
es Salaam.
Waswahili husema, hakuna kulala hadi kieleweke. Hivyo ndivyo
unavyoweza kuzungumzia mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambazo
dhahiri zimekuwa za Yanga na Azam.
Mbio hizo
zitaendelea leo kwa Yanga kuikabili Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam na Azam ikiialika Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam
Complex, Chamazi.
Timu hizo
zinafukuzana kuwania ubingwa ambao mbio zake zimegeuka vita nyingine kali
ambayo mshindi wake atasaidiwa zaidi na mbinu pia matokeo mazuri kwenye mechi
zilizosalia kabla ya kumalizika kwa msimu.
Vita nyingine
ni ya kusaka tuzo ya mfungaji bora kati ya Simon Msuva wa Yanga na Didier
Kavumbagu wa Azam.
Tayari, Msuva
amefunga mabao 11, akifuatiwa kwa karibu na Kavumbagu, mwenye mabao 10
sawa na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar katika orodha ya wafungaji bora.
Kavumbagu amekuwa
na wastani mzuri wa kufunga bao kila mechi kwa siku za karibuni, tofauti
na Msuva ambaye mara nyingi amekuwa akipoteza nafasi nyingi za kufunga.
Kabla ya mechi za
leo, Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 40, ikifuatiwa na Azam iliyoko katika
nafasi ya pili, ikiwa na pointi 36, ingawa ina mchezo mmoja mkononi.
Yanga
inaikabili Coastal ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa kwanza kwa bao
1-0, hivyo itaingia uwanjani ikijiamini kutaka kuendeleza rekodi yake nzuri
nyumbani.
Kocha Hans Pluijm
amekiri kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na uimara wa wapinzani wao,
lakini akieleza kuwa wamejipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo na mingine
iliyobakia ili kutwaa ubingwa.
Mholanzi huyo
alisisitizia wachezaji wake kuwa hawana budi kuzitumia nafasi wanazopata kwani
wao ndio chanzo cha kuinyima timu yao ushindi wa mabao.
“Ninachosisitiza
ni wachezaji wangu kutumia nafasi wanazopata, timu imekuwa ikitengeneza nafasi
nyingi, lakini umakini wa washambuliaji wangu umekuwa mdogo, hivyo wanahitajika
kuongeza umakini ili tupate mabao mengi,” alisema Pluijm.
Kocha wa muda wa
Coastal Union, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema, wamejiandaa na hawana hofu na
Yanga kwani ni kama timu nyingine yoyote, hivyo watu wasubiri kuona soka.
Chanzo:Mwananchi
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD