TANGAZO
Dar
es Salaam.Kiongozi wa Chama
cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe amesema zaidi ya wabunge 50 wa vyama
mbalimbali vya siasa nchini watajiunga na chama hicho kipya na kugombea ubunge
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Zitto ambaye
alijivua ubunge wa Kigoma Kaskazini baada ya kufukuzwa uanachama wa Chadema,
amebainisha kuwa wabunge hao, wakiwamo wa CCM na Chadema, ni miongoni mwa watu
wanaokichangia fedha chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana
na kuzinduliwa mwezi uliopita.
Pia,
amewatangazia vita wabunge wa majimbo manane ya Mkoa wa Kigoma, akijigamba kuwa
ili waweze kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo ni lazima wakubali kujiunga
na ACT kwa kuwa chama hicho kimejipanga kuyabeba majimbo yote.
Akizungumza na
waandishi wa Mwananchi katika ofisi za gazeti hili, Dar es Salaam jana, Zitto
alisema ACT ni chama kilichojipanga na ndiyo maana haikuwa ajabu katika mkutano
wake mkuu wa hivi karibuni kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 400 na kufanya
uzinduzi wa aina yake, huku akisisitiza kuwa chama hicho kinaungwa mkono na
watu wengi.
“Tuna wagombea
ubunge wengi wakiwamo wabunge wa sasa ambao katika Uchaguzi Mkuu Oktoba
hawatagombea kupitia vyama vyao vya sasa. Wapo ambao hawatakwenda hata katika
kura za maoni za vyama vyao na wameshafanya uamuzi,” alisema.
Huku akizungumza
kwa kujiamini, Zitto alisema wabunge hao ndiyo sababu ya chama hicho kuwa na
uwezo wa kujiendesha na kufafanua kuwa ACT kinawakaribisha wabunge na makada
wote kutoka vyama vya Chadema na CCM.
“Wale ambao
wanabanwa CCM na kukosa uhuru wa kuhoji jambo lolote hiki (ACT) ndicho chama
chao. Wale ambao wanaamini kuwa aina za siasa tulizotaka kuzifanya ndani ya
Chadema tukashindwa kuzifanya na wanadhani ni siasa muhimu zinazotakiwa, wapo
na sisi,” alisema.
Kuhusu Kigoma
“Nahitaji majimbo
yote ya Kigoma kuchukuliwa na ACT bila kukosa hata moja na hili hata Serukamba
(Mbunge wa Kigoma Mjini-CCM) analijua. Mwanasiasa anayetaka kuwa mbunge Kigoma
lazima aje ACT,” alisema Zitto ambaye pia alirejea kauli yake kuwa atagombea ubunge
katika jimbo jingine lakini siyo Kigoma Kaskazini.
Kauli hiyo ya
Zitto inawagusa wabunge wa sasa wa majimbo ya Kigoma ambao ni; Felix Mkosamali
(Muhambwe), Moses Machali (Kasulu Mjini), Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini)
na David Kafulila (Kigoma Kusini), wote wa NCCR-Mageuzi na Peter Serukamba
(Kigoma Mjini, Christopher Chiza (Buyungu) na Albert Obama (Manyovu) wa CCM.
Alipoulizwa iwapo
wabunge hao wa majimbo ya mkoa huo ni miongoni mwa watu watakaohamia chama
hicho alisema, “Sasa huo ni mtizamo wenu. Ukiwa mwanasiasa lazima uwe na
msingi, nataka msingi uwe Kigoma.
Tutakutana tena
kwenye chumba hiki (cha mikutano) baadaye mwezi Novemba ili mnisute kwa kauli
yangu na hapo itakuwa baada ya matokeo kutoka. Nahitaji kushinda kila kitu.
Chanzo: Mwanachi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD