TANGAZO
Na Christopher Lilai, Nachingwea,
Vijana wilayani Nachingwea mkoa wa Lindi wameamua kuhamasishana kwa kutoa elimu
ya uraia na umuhimu wa upigaji kura kwa wananchi hasa wanawake na vijana
ili wajitokeze katika upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Hatua ya vijana hao imetokana na kuonekana kuwa vijana wengi wamekuwa
hawajitokezi kwenye upigaji wa kura kwenye chaguzi zilizopita hali iliyofanya
takwimu ya waliopiga kura kuwa ndogo ikilinganishwa na idadi ya waliojiandikisha.
Akizungumza hivi karibuni na Blog ya Mtazamo Mpya kwa niaba ya vijana wa kata
kumi za wilayani Nachingwea ambao wameunda vilabu vya vijana kwenye kata
,Teresia Makota mkazi wa kijiji cha Matangini,kata ya Nangoe alisema lengo la kuanzisha vilabu hivyo ni
kuwahamasisha vijana na wanawake ili wajitokeze katika upigaji kura kwenye
uchaguzi mkuu na kura ya maoni ya katiba iliyopendekezwa na pia wagombee
nafasi mbalimbali za uongozi.
Alibainisha kuwa tafiti mbalimbali zimebaini na kuthibitisha bila shaka kuwa
vijana wanahitaji kushiriki na kushirikishwa ili wajisemee kuhusu haki zao za
msingi.
“Sisi vijana bila kujali itikadi zetu za kisiasa tumeamua kuanzisha
vilabu ambavyo vitatuunganisha kwa lengo la kuchagua viongozi ambao watajali
maslahi yetu”alisema Teresia.
Kwa upande wake Jackson Juma mkazi
wa kijiji cha Mandawa,kata ya Ruponda alisema kupitia vilabu hivyo vijana
wamepata jukwaa na kuzungumza na kutoa mawazo yao bila kuingiliwa na itikadi ya
vyama vya siasa wa dini na kuwa itaongeza uelewa kwa kundi hilo kujitambua.
Alibainisha kuwa vilabu hivyo vimekuwa na fursa ya kumfanya kijana hasa wa
kijijini kupata uelewa wa mambo mbalimbali yanayoendelea na yale
yatakayoendelea yenye maslahi kwa taifa.
Naye Juma Alli mkazi wa mtaa wa uhindini kata ya Nachingwea alisema kuwa
kupitia vilabu hivyo vijana watapata uelewa katika masuala mazima yanayogusa
mstakabali wa vijana hasa katika upatikanaji wa ajira.
Mratibu wa mradi huo Sharifu Maloya,alisema mradi huo unaofahamika kwa
jina la fahamu,ongea,sikilizwa (FOS11) unatekelezwa kwenye mikoa 20 ya Tanzania
bara na visiwani ambao unawalenga vijana na wanawake na jamii kwa ujumla ambapo
utaongeza ari na uwezo wa wananchi kuwa wapiga kura na waangalizi wa uchaguzi.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD