TANGAZO
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na ya
kustaajabisha mwalimu mkuu wa shule ya
Msingi Mkutingome,kata ya Mbekenyera Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoani
Lindi Hemed Ismail Nambea amekuta jeneza likiwa limefunikwa shuka nyeupe katikati
ya mlango nje ya nyumba yake.
Jeneza lililotumika na kuwekwa nje ya nyumba ya
mwalimu huyo ni hilo hilo ambalo hutumika kwa ajili ya
shughuli za mazishi ya kawaida kijijini
hapo ambapo watu hao wanadaiwa kwenda kulichukua jeneza hilo msikitini usiku.
Tukio hili limetokea usiku wa kuamkia leo
kijijini hapo kwa kile kinachodaiwa kuwa mwalimu huyo kushindwa kwake kuzuia suala la wanafunzi wa shule hiyo
kudondoka ovyo wakiwa shuleni huku wazazi wa watoto hao wakidai kuwa chanzo cha
tatizo hilo ni yeye wakiwa na imani za kishirikina dhidi ya mwalimu huyo.
Tuhuma zingine ambazo wananchi wa kijiji cha
Mkutingome wanamtupia mwalimu huyo ni kwamba tatizo la watoto wao kuendelea
kusumbuliwa na ugonjwa huo kunachangiwa nay eye ingawa walishindwa kueleza ni
kwa namna gani mwalimu huyo anakwamisha zoezi la wanafunzi hao kupewa dawa za
tiba za asili na hatimaye kupona.
Ugonjwa huo wa ajabu kwa mara ya kwanza uliibuka shuleni hapo
mwanzoni mwa mwaka jana ambapo licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na walimu hao
kutoa elimu kwa wanakijiji hao lakini bado baadhi ya wazazi wa watoto hao
wamekuwa wakiwatupia lawama walimu hao.
Akizungumza na Blog ya Mtazamo Mpya hii leo Mwalimu
huyo alisema kuwa ni kwa muda mrefu sasa amekuwa akiishi kwa shida na hofu kijijini
hapo kutokana na vitisho vya kuuawa anavyopewa na wana kijiji hao mazingira
yanayopelekea kushuka kwa morari yake ya utendaji kazi zake za ufundishaji.
Alisema kutokana na tatizo hilo uongozi wa
shule hiyo pamoja na uongozi wa serikali ya kijiji walifanya kikao shuleni hapo
wiki iliyopita ili kujadili mustakabali wa wanafunzi sita ambao bado tatizo la kuanguka
linawakabili na makubaliano yakawa ni kuwaondoa kwa muda wanafunzi hao shuleni
hapo ili wakapate tiba.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo alisema wiki moja iliyopita
April 16 mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku akiwa anajiandaa kwenda kuangalia mechi kati
ya timu ya Barcelona na PSG alikuta
maneno ya makali mlangoni pake ya
kumtahadharisha yaliyosema “Hatuna imani na wewe mwalimu mkuu juu ya uangukaji
wa watoto shuleni kwa hiyo tunakupa siku mbili uamishe kambi bila ubishi na
ukiwa mbishi utakachokiona usishangae tumechoka na mambo yako”.
Alisema baada ya kuona maneno hayo yaliyomtisha
alitoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji ambapo alihaidiwa na ofisa
mtendaji wa kijiji hicho kuwa tatizo lake watalishughulikia kwa kuwatafuta wote
waliohusika na kufanya kitendo hicho ambacho si cha kiungwana.
Aidha mwalimu huyo alidai kuwa huku akisubiri
hatima ya suala hilo la kukuta maandishi ya vitisho mlangoni kwake leo asubuhi
watoto wake walipofungua pazia ya chumba chao wanacholala waliona kitu kikiwa
kimefunikwa shuka nyeupe nje ya nyumba yao na ndipo walipomwamsha na alipotoka
nje alikuta jeneza hilo ambalo hakujua ni kwa nini liko hapo na nani amelileta.
Alisema aliamua kutoa taarifa kwa majirani na
uongozi wa serikali ya kijiji ambapo walipofika walilifunua jeneza hilo la
kukuta mifuko ya plastiki inayowekwa nje ya magodoro ya Dodoma yakiwa
yamefinywanga pamoja mithili ya kichanga kilichokufa.
Kwa upande wake ofisa mtendaji wa kijiji cha
Mkutingome Mussa Bakari Mbulinda alisema
kuwa ni kweli mwalimu huyo amekuwa akitishiwa maisha kila siku kijijini hapo na
kwamba tuhuma wanazodai kuwa mwalimu huyo ni mshirikina si za kweli na kwamba
wameamua kuitisha mkutano mkuu wa kijiji utakaofanyika siku ya jumatatu April
27 mwaka huu.
Alisema ukweli ni kwamba usalama wa mwalimu
huyo uko kwenye mazingira hatarishi na kumuomba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
hiyo afanye uhamisho wa mwalimu huyo huku akikiri kuwa hata walimu wengine
waliopo kijijini hapo ambao ni wageni waliokuja kuanza kazi kijijini hapo
wanaona ni vyema nao wahamishwe wakihofia usalama wa maisha yao na familia zao.
Taarifa za ndani zaidi zinadai kuwa baada ya
wanakijiji hao kuona siku walizompa mwalimu huyo aondoke kijijini hapo zimepita
waliamua kumletea jeneza ikiwa ni ujumbe kwake kuwa ameshindwa kuondoka kwa
ridhaa yake basi ataondoka bila ridhaa yake akiwa ndani ya jeneza.
MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Mkutingome Kata ya Mbekenyera Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi Hemed Ismail Nambea ambaye amekumbwa na kadhia hiyo ya kukuta jeneza nje ya Nyumba yake.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD