TANGAZO
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Sekretarieti ya ajira katika
Utumishi wa umma inatarajia kuzindua mfumo mpya wa utumaji na upokeaji wa
maombi ya kazi kwa njia ya mtandao kupitia “Recruitment portal” hivi karibuni
baada ya hatua za majaribio ya mfumo huo kuonyesha mafanikio.
Sababu za kuanzisha mfumo huu mpya zinalenga kuboresha utendaji kazi wa taasisi
katika kufikisha huduma kwa wateja, kuongeza ufanisi katika mchakato wa ajira,
Kupunguza muda wa mchakato wa Ajira ili kukidhi mahitaji ya wadau, kuwafikia
waombaji wa nafasi za kazi wengi zaidi, kudhibiti udanganyifu wa sifa toka kwa
waombaji wa fursa za Ajira kwa kurahisisha ukaguzi na uhakiki wa taarifa za
waombaji kazi kwa kuunganishwa na mifumo ya taasisi mbalimbali lakini pia
kukidhi maelekezo ya Sera mbalimbali za utumishi wa umma pamoja na dira ya
Taifa ya mwaka 2025 kuhusiana na umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano katika kutimiza malengo ya Taifa.
Hadi sasa Sekretarieti ya ajira imefanya majaribio ya kupokea maombi ya kazi
kwa kutumia mfumo wa “Recruitment Portal” kwa matangazo ya kazi matano ambayo
yaliyowahusu waajiri mbalimbali serikalini na muitikio umeonekana kuwa mzuri.
Matangazo
hayo yalihusu Wakala wa serikali mtandao lililotolewa tarehe 22 Aprili, 2014
ambapo kati ya nafasi 12 zilizotangazwa idadi ya maombi yaliyopokelewa yalikuwa
1,158, Tangazo la nafasi za Mkemia mkuu wa Serikali lililotolewa tarehe 4
Desemba, 2014 lenye nafasi 11 jumla ya maombi ya kazi 119 yalipokelewa kwa njia
ya mtandao. Matangazo mengine ni ya Mamlaka ya Hali ya hewa la tarehe 4
Desemba, 2014 lililokuwa na nafasi moja na idadi ya maombi ya kazi matatu
yaliyopokelewa, tangazo la tarehe 16 Januari, 2015 la Wizara ya Ardhi
lililokuwa na nafasi 51 ambalo jumla ya maombi ya kazi 738 yaliwasilishwa na
tangazo la mwisho lilitolewa tarehe 10 Machi, 2015 kwa niaba ya taasisi
mbalimbali Serikalini jumla ya maombi ya kazi 2,567 yalipokelewa kutumia mfumo
huu. Idadi hii inaonyesha kuwa watu wengi wameanza kuhamasika na matumizi ya
mfumo huu.
Taratibu za uzinduzi rasmi wa
mfumo huu inatarajiwa kufanyika hivi karibuni ambapo sekretarieti ya ajira
inatarajia kupunguza muda wa uendeshaji wa mchakato wa ajira kwa asilimia 34%.
Aidha mfumo pia utapunguza changamoto kadhaa zikiwemo baadhi ya barua kutofika
kwa wakati au kupotea kwa kutumia njia ya posta, Mrundikano wa barua na nyaraka
nyingine zinazohusiana na maombi ya kazi kutokana na matumizi ya karatasi,
Barua za vibali vya ajira kuwasilishwa wakati vimechelewa na kusababisha
mchakato kuchelewa na gharama inayotokana na uendeshaji wa mchakato mzima wa
ajira kuwa juu. Pia mfumo huu utakuwa rafiki na rahisi kwa watumiaji kwa kuwa
wataweza kutumia simu zao za kiganjani kupata taarifa za mchakato wa ajira kila
wakati kwa kupiga *152*00#
Tunatoa rai na kusisitiza kuwa
waombaji kazi na wale wanaotarajia kuingia katika soko la ajira wajisajili
katika mfumo huu kwa kufunguahttp://portal.ajira.go.tz ili kuingiza taarifa zao za kitaaluma,
wasifu binafsi (CV) pamoja na vyeti. Matarajio ya Sekretarieti ya ajira ni
kuona kuwa mara baada ya mfumo huu kuzinduliwa rasmi utaongeza ufanisi, ubora,
uwazi na uwajibikaji wa huduma zinazotolewa, kupunguza muda unaotumika sasa wa
kuendesha mchakato wa ajira, Gharama za uendeshaji zitapungua kwa kiasi kikubwa
na mfumo utawafikia waombaji wa fursa za kazi wengi zaidi na kwa haraka.
Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma inapenda kuwasisitiza wananchi hususani waombaji kazi kuwa
inaendelea na uimarishaji wa mfumo mpya wa kutuma maombi ya kazi kwa njia ya
mtandao (recruitmemnt portal) ili kuondoa baadhi ya changamoto zilizojitokeza
baada ya majaribio kabla ya uzinduzi wake na tunasisitiza na kuhimiza waombaji
kazi pamoja na wanafunzi wanaotarajia kumaliza vyuo waendelee kujisajili katika
mfumo huo mpya.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi
ya Rais Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD