TANGAZO
BAADHI ya maeneo ya utengenezaji wa Madawati katika kituo cha Wapiwapi mjini Masasi.
Na
Clarence Chilumba,Masasi.
HALMASHAURI
ya mji wa Masasi mkoani Mtwara imefanikiwa kukamilisha utengenezaji wa Madawati
kwa shule za msingi na sekondari kwa
asilimia 80 hadi sasa huku jitihada zingine za kukamilisha zoezi hilo ifikapo
Juni 30, 2016 zikiwa zinaendelea.
Hadi sasa jumla ya
madawati 1446 tayari yameshatengenezwa kati ya madawati 2329 yaliyohitajika kwa shule 32 za msingi za Halmashauri hiyo
ambapo madawati 883 yaliyobakia tayari mbao zimeshapatikana huku utengenezaji
wa madawati hayo ukiwa mbioni kukamilika mwishoni mwa wiki hii.
Akizungumza kaimu
mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Masasi Geofrery Martin alisema kwa sasa ili
kukamilisha kwa wakati zoezi hilo wameweka vituo vitano vya utengenezaji wa
madawati hayo ambavyo ni pamoja na Nyasa,Wapiwapi,Mkuti,Wabiso pamoja na
Kisiwani.
Alisema katika vituo
hivyo vitano kituo cha Nyasa kinatarajia kutengeneza jumla ya madawati 224
ambapo kati ya hayo 73 ni kwa ajili ya shule ya msingi Maendeleo na 151 ni kwa
ajili ya shule ya msingi Nyasa na kituo cha Wapiwapi kitatengeneza madawati 177
kwa ajili ya shule ya msingi Kambarage.
Aidha katika kituo
cha Mkuti kinatarajia kutengeneza madawati 166 kwa ajili ya shule ya msingi
Mkuti,Kituo cha Kisiwani Madawati 166 kwa ajili ya shule ya msingi Sabasaba na
katika kituo cha Wabiso kitatengeneza madawati 152 kwa ajili ya shule ya msingi
Mkomaindo.
“Tuko katika hatua
nzuri ya umaliziaji wa zoezi la utengenezaji wa madawati kwa shule zetu za
msingi…kwa sasa tulichofanya ni kugawa kazi katika vituo mbalimbali vya
utengenezaji na tunaamini ifikapo jumapili wiki hii tutakuwa tumekamilisha
zoezi hili”.Alisema Martin.
Alisema Kutokana na kuwepo kwa mpango
wa elimu bila malipo wazazi mjini humo
walijitokeza kwa wingi kupeleka watoto
wao shuleni mazingira ambayo yalisababisha
kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi kwenye shule za msingi ambapo jumla ya
wanafunzi 20,957 waliandikishwa kuanza darasa la kwanza.
Alisema kutokana na idadi kubwa ya
wanafunzi kuandikishwa kwenye shule zote zilizopo katika Halmashauri hiyo kumekuwa
na changamoto kubwa kwa baadhi ya shule hizo kwa wanafunzi wake kukaa chini
kutokana na upungufu wa madawati.
Katika hatua nyingine kaimu mkurugenzi
huyo wa Halmashauri ya mji wa Masasi alisema tayari zoezi la utengenezaji wa
viti pamoja na meza 778 kwa shule 10 za sekondari za halmashauri hiyo
umekamilika na tayari wameshasambaza mashuleni.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara Mheshimiwa Sospeter Nachunga (Kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Fundi anayetengeneza Madawati hayo katika kituo cha Wapiwapi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD