TANGAZO
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amesema Serikali imeagiza kutoka nje ya nchi tani 70,000 za sukari
ambapo kati ya hizo, tani 11,957 zimeshawasili nchini na zitaanza kusambazwa
kesho (Jumatano).
Ametoa kauli hiyo leo
mchana (Jumanne, Mei 10, 2016) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye
mkutano uliofanyika nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Akitoa ufafanuzi wa
sukari ambayo imekwishawasili nchini, Waziri Mkuu alisema tani 2,000
zitapelekwa mikoa ya Kaskazini, tani 3,000 (mikoa ya Kanda ya Ziwa), tani 2,000
(mikoa ya Kusini), tani 2,000 (Nyanda za Juu Kusini) na tani 2,000 (mikoa ya
Kanda ya Kati).
“Tani nyingine 24,000 za
sukari zitawasili Ijumaa hii na hadi zitoke bandarini itakuwa kama Jumapili kwa
hiyo zinaweza kusambazwa kuanzia Jumatatu. Tani nyingine 20,000 zitawasili
baadaye, ama mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi Juni,” alisema Waziri Mkuu.
Amesema anawataka
Watanzania wasihofu kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza hivi karibuni kwani
umesababishwa na watu wachache.
“Mheshimiwa Rais ameagiza watu waliohodhi
bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe. Lakini pia tunaagiza kwa muda mfupi
kwa sababu viwanda vyetu vinatarajia kuanza uzalishaji ifikapo Julai,” alisema.
Amewataka wasambazaji wa
sukari waziuze kwa wafanyabishara wadogo ili wao wawawuzie wananchi kwa bei
elekezi ya sh. 1,800. Pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya
kuhakikisha wanasimamia zoezi la ukaguzi ili kubaini zaidi wale waliohodhi
bidhaa hiyo.
Akifafanua kuhusu mkakati
wa Serikali kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, Waziri Mkuu amesema nia ya
Serikali ni kuhakikisha tatizo la uhaba wa sukari nchini linakwisha ifikapo
2019. “Wananchi wasiogope, Serikali imechukua hatua kwa udhibiti mzuri ili
tusije kuporomosha soko letu la ndani,” alisema.
“Tunao mkakati wa
kuboresha viwanda vya ndani, wenye viwanda wenyewe au kwa ubia na wawekezaji
kutoka nje, wanaweza kufungua mashamba kwenye maeneo matatu tuliyotenga kwa
ajili hiyo,” alisema.
“Serikali imetenga maeneo
matatu yanayofaa kwa kilimo cha miwa huko Bagamoyo, Ngerengere na Kigoma. Huko
wanaweza kulima na kujenga viwanda vya sukari na uzalishaji ukawa unapanda
mwaka kwa mwaka hadi tutakapoweza kuimaliza hii gap iliyopo,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
OFISI YA WAZIRI MKUU
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
JUMANNE, MEI 10, 2016.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD