TANGAZO
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Masasi,Fortunatus Mathew Kagoro (Picha ya Maktaba).
TAARIFA
FUPI KUHUSU HALI YA MADAWATI HALMASHAURI YA MJI WA MASASI.
Katika kutekeleza agizo
la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk.John Pombe Magufuli alilolitoa Machi 16,2016 wakati anawaapisha
wakuu wa mikoa kuhusu utekelezaji wa
elimu bila malipo,Rais aliwataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanasimamia upatikanaji
wa madawati ifikapo Juni mwaka huu.
Mkoa wa Mtwara chini ya uongozi wa mkuu wa mkoa huo Mheshimiwa Halima
Dendego umedhamiria kukamilisha suala la madawati ifikapo Mei 2016 kwa
Halmashauri zote tisa zinazounda mkoa huo Masasi mji ikiwemo kutumia njia
mbalimbali ili wanafunzi wote wakae kwenye madawati.
Katika kikao kilichoitishwa Februari, mwaka huu na mkuu wa mkoa
wa Mtwara baada ya kubaini changamoto
hizo, wakurugenzi wa halmashauri na
wakuu wa wilaya waliagizwa kuhakikisha wanashughulikia changamoto hizo hasa uhaba wa madawati ambapo kwa ujumla mkoa wa Mtwara una upungufu wa
madawati 35,406.
Kwa upande wa Halmashauri ya mji wa Masasi tayari mchakato wa
upatikanaji wa madawati hayo umeanza kwa kutumia rasilimali zilizopo pamoja na
mapato ya ndani sambamba na kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo zikiwemo
taasisi za serikali,taasisi binafsi za kifedha,wafanyabiashara pamoja na
wananchi wote kwa ujumla kwa lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo Mei 2016 watoto
wote wanaokaa chini wawe wamepata madawati.
HALI HALISI:
Kutokana na kuwepo kwa mpango wa elimu bure bila malipo wazazi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi
kupeleka watoto shule mazingira yaliyopelekea kuwepo kwa idadi kubwa ya
wanafunzi kwenye shule za msingi na sekondari ambapo kwa upande wa shule za
msingi jumla ya wanafunzi 20,957 waliandikishwa kuanza darasa la kwanza.
Aidha kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kuandikishwa kwenye shule
zote 33 zilizopo katika Halmashauri hiyo kumekuwa na changamoto kubwa kwa
baadhi ya shule hizo wanafunzi wake kukaa chini kutokana na uhaba wa madawati.
Halmashauri ya mji wa Masasi inahitaji jumla ya Madawati 6975,huku
yaliyopo ni madawati 4646 na pungufu ni madawati 2329 hivyo ili wanafunzi wote
waweze kukaa kwenye madawati Halmashauri inahitaji kiasi cha shilingi Milioni
349,350,000 ambapo hadi sasa kazi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Halmashauri
katika kutatua changamoto hiyo ya madawati.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA HALMASHAURI:
Halmashauri ya mji wa Masasi imefanya jitihada mbalimbali katika kukabiliana
na changamoto hiyo ya upungufu wa madawati na miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na:
- · Kuanzisha Kampeni inayoitwa “ONA AIBU MTOTO WAKO KUKAA CHINI SHULENI…JITOLEE KUTENGENEZA DAWATI…MASASI NI MIMI NA WEWE”.
- · Upasuaji wa Mbao na Boriti kwa kutumia miti iliyopo eneo la Halmashauri ambapo hadi sasa jumla ya mbao 119 pamoja na Boriti 65 zimepatikana.
- · Kuandika barua za maombi ya mchango kwa vyama vya ushirika vilivyopo Halmashauri ya mji wa Masasi.
- · Maombi kwa taasisi za kifedha ikiwemo NMB ambao wameahidi kutengeneza madawati kwa awamu tano na kwa awamu ya kwanza watatengeneza madawati kwa shule moja ingawa hawakueleza idadi ya madawati wataakayotengeneza.
- · Kuomba mchango kwa Wakala wa huduma za misitu kanda ya kusini (TFS) ambao wamekubali kutoa msaada wa madawati 40 ambayo tayari yameanza kutengenezwa.
- · Mazungumzo kati ya Halmashauri na wafanyabiashara wa mazao mchanganyiko ambao wamekubali kuchangia kiasi cha shilingi 10 kwa kila kilo moja wakati wa ununuzi wa mazao hayo.
Kwa upande wa idara ya elimu sekondari pia kumekuwepo na changamoto
kadhaa za elimu kwenye shule zake Tisa (9) zilizopo kwenye Halmashauri ya mji
wa Masasi ambapo kwa sasa changamoto kubwa iliyopo ni upungufu wa viti na
madawati.
Mahitaji ambayo kwa sasa yanahitajika ni pamoja na meza 3664,viti 3664
na kwamba meza zilizopo ni 3078 na viti 2657 huku upungufu ukiwa ni meza 586 na viti 1007. Kushuka kwa
upungufu huu ni kutokana na juhudi za Halmashauri za kukarabati viti na meza
mbovu.
WITO:
Hivyo ukiwa kama mdau wa elimu tunaomba msaada wako wa hali na mali
katika kuhakikisha kero hii ya madawati kwa watoto wetu ambao baadhi yao
wamekuwa wakikaa chini kwa kukosa madawati inakwisha ili kutekeleza agizo la
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli.
Ujumbe: “ONA AIBU MTOTO WAKO KUKAA CHINI SHULENI…JITOLEE
KUTENGENEZA DAWATI…MASASI NI MIMI NA WEWE”.
Clarence Chilumba,
Ofisa Habari Halmashauri ya Mji Masasi,
03/04/2016.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD