TANGAZO
Christopher Lilai,Nachingwea.
Wanufaika wa mpango wa
kunusuru kaya maskini wilayani Nachingwea, mkoani Lindi wamekiri kuwa mpango
huo umekuwa mkombozi mkubwa kwao kwani umeweza kuwabadilisha kimaisha na
kuiomba serikali kuongeza kiwango cha ruzuku ili kilingane na thamani halisi ya
fedha kwa sasa.
Wakizungumza kwa jana nyakati
tofauti na timu ya waandishi wa habari waliotembelea baadhi ya wanufaika hao walisema
kiwango kinachotolewa ni kidogo sana ambacho pia kinatolewa kila baada ya miezi
mitatu hivyo serikali ione uwezekano wa
kuongeza kiwango hicho na kutolewa kila mwezi.
Samson Nachuruchonga
ambaye ni mlemavu wa viungo wa kijiji cha Ntila alisema licha ya kiwango
wanachopata kuwa kidogo kimeweza kuwasaidia kugharamia mahitaji muhimu ikiwemo
chakula,kusomesha watoto wake kwa kuwanunulia sare na vifaa vya shuleni.
Alisema pia anazitumia
fedha hizo kwa kilimo kwani kwa sasa anaweka watu shambani na kuwalipa hivyo
kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na kutumia fedha
zinazopatikana kupitia kilimo kujijengea nyumba ya bati.
Naye Zainabu Mpunga (73)
mkazi wa kijiji cha Chiganga ambaye licha ya kuwa mjane pia anatunza wajukuu
wake wawili ambao ni watoto wa marehemu binti yake alisema kuwa ameanza ujenzi
wa nyumba kwa kununua bati moja moja kila anapopata ruzuku hiyo na kuwa
anatarajia mwaka huu anaratajia kuanzisha ujenzi huo.
Kwa upande wake mratibu
msaidizi wa TASAF wilayani Nachingwea,mkoani Lindi, James Mbakile, alisema kuwa
kutokana na mpango huo baadhi ya wanufaika wameweza kubadilisha maisha yao kwa
kujianzishia miradi midogo midogo ikiwemo ufugaji wa kuku wa kienyeji, nguruwe
na mbuzi na kujijengea nyumba za kisasa.
Alisema kuwa jumla ya
shilingi Bilioni 2.3 zimenufaisha kaya 5,850 katika vijiji 69 vya wilayani
Nachingwea kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini tangu kuanza mpango huo
ambao wanufaika wake ni kaya za wazee wasiojiweza na wale wanye magonjwa sugu
wamekuwa wakishauriwa kutumia fedha hizo chache kwa kujitafutia
chakula,kugharamia masomo na matibabu.
Aidha Afisa mshauri wa
kitaalamu wa TASAF wa wilaya hiyo, Dorothy Shiyo aliwaomba viongozi wa serikali
za vijiji wawe wasimamizi wa karibu kwa kuwasimamia wananchi kutumia fedha
wanazozipata kwa manufahaa ikiwa ni pamoja na kujiwekea akiba.
“Serikali za vijiji
viweke washauri wa kwanza katika matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa hivi sasa”alisema Shiyo.
Shiyo aliwaomba walengwa
wa mpango huu katika kipindi hiki ambapo kaya nyingi zinakabiliwa na tatizo la
chakula kutimia fedha hizo kujinunulia chakula.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD