Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

MWENYEKITI CHADEMA MKOA WA MTWARA ASISITIZA MAKAIDI NI MGOMBEA HALALI JIMBO LA MASASI KUPITIA UKAWA

TANGAZO
 Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na maendeleo Chadema Mkoa wa Mtwara Kassim Bingwe (Kushoto) aliyeshika karatasi yenye maneno Time For Change.
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Baada ya mvutano wa muda mrefu wa vyama vinavyounda Umoja wa Ukawa wa kuachiana majimbo wilayani Masasi hatimaye  mwenyekiti wa chama cha demokrasia na maendeleo Chadema mkoa wa  Mtwara Kassim Bingwe ameweka wazi msimamo wa chama chake kuwa  mgombea halali wa umoja huo kwa nafasi ya ubunge jimbo la Masasi ni mwenyekiti  mwenza wa Ukawa Dkt.Emanuel Makaidi.

Aliyasema hayo jana  wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama cha NLD ambacho mwenyekiti wake wa taifa  ni Dkt.Makaidi na  anagombea nafasi ya ubunge jimbo la Masasi kupitia Ukawa uzinduzi uliofanyika   kwenye viwanja vya Terminal two maarufu uwanja wa fisi.

Alisema  baadhi ya viongozi  wa vyama vinavyounda umoja huo wamekuwa wakimbeza Dkt.Makaidi na kuonesha dharau dhidi yake na kwamba wanaofanya vitendo hivyo ni dhahiri hawamjui Makaidi na hawajui Siasa na mchango mkubwa alionao kwenye umoja wa katiba ya wananchi Ukawa.

Alisema wananchi wa wilaya ya Masasi pamoja na viongozi wote wa Ukawa wanapaswa kumuunga mkono Makaidi katika harakati zake za kuomba ridhaa kwa wananchi wa jimbo la Masasi ili aweze kushinda kwenye uchaguzi mkuu ujao oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa Chadema mkoa wa Mtwara alisema kitendo kinachofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo wilayani humo cha kumkejeli na kumkataa Makaidi tena mbele ya viongozi wa juu wa Ukawa ni kuirahisishia CCM ili iweze kupata ushindi wa kishindo.

“Ndugu zangu wana Ukawa Wilayani Masasi mnachopaswa kufahamu ni kuwa Dkt.Emanue Makaidi ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa…lakini pia ni miongoni mwa wanasiasa wakongwe nchi hii hivyo mnapaswa kumuheshimu kama baba yenu kwenye majukwaa ya kisiasa na kwamba hiki mnachofanya hakipaswi kuachwa kikiendelea”.alisema Bingwe.

Aidha Bingwe amewajia juu baadhi ya viongozi wa umoja huo wilayani hapa wanaohoji  uhalali wa Makaidi kugombea ubunge jimbo la Masasi kwa kigezo kuwa maisha yake ni Dar es salaam huku akihoji kuwa mbona mwenyekiti wa Chadema taifa Kamanda Freeman Haikael Mbowe anaishi Dar es salaam lakini ni mbunge wa Hai na wananchi wake wamemkubali?

Alisema makubaliano ya Ukawa ni kuachiana majimbo na sio kushindanisha wagombea kama baadhi ya watu wanavyosambaza uvumi kuwa Ukawa wamekubaliana kushindanisha wagombea na kuangalia mgombea gani anakubalika au anashangiliwa sana na wananchi wa eneo husika.

Alisema ukweli ni kwamba Dkt.Emanuel Makaidi ndie mgombea halali na anayetambulika na umoja wa Ukawa na kwamba hao wagombea wengine wanaoendelea na mchakato wa kampeni ndani ya jimbo hilo wanajidanganya na kupoteza muda wao huku akiapa mbele ya maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa chama chake kitatoa ushirikiano wakati wote wa kampeni za Dkt.Makaidi.

 Kassim Bingwe akiwa kwenye moja ya mikutano ya kuimarissha chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema wilayani Masasi katika eneo la Mti Mwiba.

Katika jimbo la Masasi viongozi wa umoja huo  wamevunja makubaliano waliyoyaweka wenyewe huku kila chama kikisimamia msimamo wake kwa kusimamisha mgombea ingawa makubaliano ya umoja wa ukawa ngazi ya juu na yaliyosainiwa na viongozi wa umoja huo taifa jimbo la Masasi wameachiwa Chama cha NLD.

Mvutano mkubwa uliopo ni kati ya mgombea wa chama cha NLD Dkt.Emanuel Makaidi na mgombea wa CUF Ismail Makombe (Kundambanda) ambaye anaonesha kuungwa mkono na wanachama wa vyama vinavyounda umoja wa Ukawa wilayani humo.

Katika hatua nyingine mara baada ya mkutano huo,habari leo ilimtafuta katibu wa chama cha wananchi CUF wilaya ya Masasi Hassan Chaliche  ili aweze kueleza msimamo wake juu  ya mvutano huo na kusema kuwa kwa hali ilivyo sasa Ukawa Masasi uko kwenye mgogoro mkubwa.

Alisema kuwa mgombea wao wa CUF Ismail Makombe ataendelea kufanya kampeni kwani yeye ndie anayekubalika na wananchi wa Masasi na kwamba kauli iliyotolewa na mwenyekiti huyo wa Chadema hawakubaliani nayo.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi ni kwa nini anakinzana na makubaliano yaliyosainiwa na viongozi wao wa juu na kutolewa kwa vyombo vya habari Chaliche alisema wao wamepokea maagizo kutoa kwa uongozi wa juu wa CUF kuwa mgombea wao aendelee na mchakato wa uchaguzi ndani ya jimbo hilo.


Septemba mosi mwaka huu mgombea  mwenza wa urais kupitia umoja unaounda Ukawa Juma Duni Haji  alishindwa kumaliza mgogoro unaoendelea katika jimbo la Masasi kuhusu nani mgombea ubunge rasmi anaegombea kupitia umoja huo.


Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wananchi wanaodhaniwa kuwa na mapenzi wa mgombea wa CUF Ismail Makombe kuanza kuzomea jukwaa kuu la viongozi wa umoja huo akiwemo Duni na hatimaye mkutano huo kuvunjika na vijana kuingia barabarani wakiimba nyimbo za kumkataa Makaidi na kumkubali Kundambanda.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top