Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

HIVI NDIVYO MAGUFULI ALIVYOITIKISA NANYUMBU NA MASASI,MAELFU YA WANANCHI WAJITOKEZA KUMSIKILIZA

TANGAZO
 Maelfu ya wananchi wa wilaya ya Masasi wakimsikiliza mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM Dkt.John Pombe Magufuli kwenye viwanja vya Bomani Mjini Masasi jana.

Na Clarence Chilumba,Masasi.
MGOMBEA wa nafasi ya urais kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Dkt.John Pombe Magufuli ameendelea kuwaomba watanzania wamuamini kwa kumpa kura za ndio kwenye uchaguzi mkuu ujao oktoba mwaka huu huku akiwahaidi kuwa kamwe hatowaangusha.

Aliyasema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati anawahutubia maelfu ya wananchi wa wilaya za Nanyumbu na Masasi mkoani Mtwara  waliojitokeza kumsikiliza akiwa kwenye muendelezo wa kunadi sera za CCM.

Alisema watanzania wasirubuniwe na ahadi hewa zinazotolewa na kwamba yeye yuko tayari kubadilisha maisha ya watanzania endapo watampa ridhaa ya kuwatumika katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema anafahamu kuwa watanzania wana kiu ya mabadiliko na hata yeye pia anahitaji mabadiliko na kwamba mabadiliko ya kweli yatapatikana kwa kumpa kura za ndio yeye pamoja na chama cha mapinduzi kwa ujumla.

 Wananchi wa wilaya ya Nanyumbu waliojitokeza kumsikiliza Dkt.John Pombe Magufuli.


Kwa mujibu wa Dkt.Magufuli alisema kote alikopita ameshuhudia changamoto mbalimbali zinazowakabili watanzania ikiwemo maji,afya,barabara,kilimo huku akiwaahidi kuwa serikali yake itahakikisha kero hizo zinabaki kuwa historia.

Akizungumzia zao la korosho ambalo limekuwa na chagamoto nyingi kwa siku za hivi karibuni Dkt. Magufuli alisema anafahamu umuhimu wa zao hilo kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara na kwamba anayo dhamira ya dhati kutoka moyoni mwake kumaliza matatizo yote yanayoathiri mfumo mzima wa zao la korosho endapo watampa ridhaa.

“Nafahamu namna zao la korosho linavyoyumba wakati wa ununuzi…nipeni kura za ndio kwenye uchaguzi mkuu ujao baadae oktoba mwaka huu hakika naapa mbele yenu kuwa korosho itakuwa juu na kila mwana Mtwara na Lindi atakuwa na hamu ya kulima zao hilo”.alisema Magufuli huku akishangiliwa.


 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara Mohamed Sinani akiongea na wananchi wa mji wa Masasi kabla ya kumkaribisha Dkt.John Pombe Magufuli kuongea na wananchi hao.
 Dkt.John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa wilaya ya Masasi waliojitokeza kumsikiliza kwenye viwanja vya Boma.

Aidha Dkt.Magufuli amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Masasi kuwa endapo watampa kura za ndio tatizo la umeme linaloikabili wilaya hiyo litakwisha kwa kuboresha miundo mbinu iliyo chakavu pamoja na kuongeza watumishi wa shirika hilo wilayani humo.

Alisema watanzania wanapaswa kufanya maamuzi sahihi na yenye tija kwa vizazi vijavyo na kwamba watazame baadhi ya nchi zilizofanya mabadiliko yaliyotokana na shinikizo na mataifa ya magharibi ikiwemo Libya ambayo kwa sasa wananchi wake wanaishi maisha ya shida yasiyo na furaha.

 Wananchi wa wilaya ya Masasi wakipunga mikono kwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM Dkt.John Pombe Magufuli jana.


“Ndugu zangu wana Masasi mabadiliko hakuna asiyependa wote tunapenda hata mimi hapa ni muumini wa mabadiliko…lakini ni mabadiliko gani tunafanya? Angalieni ndugu zetu wa Libya hadi sasa hali ni tete tatizo ni hayo hayo mabadiliko msikubali kudanganywa”.alisema Magufuli.


Dkt.John Pombe Magufuli yuko mkoani Mtwara akiendelea na harakati zake za kuwafikia watanzania wote nchini akiomba kura za ndio yeye,wabunge pamoja na madiwani wa CCM ili waweze kuwatumikia wananchi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.


 WAGOMBEA wa nafasi za udiwani kupitia CCM wilaya ya Masasi wakipunga mikono wakati mgombea wa Urais kupitia chama cha mapinduzi Dkt.John Pombe Magufuli akiwasili kwenyen viwanja vya Boma Mjini Masasi.


Wananchi wa wilaya ya Masasi wakiwa kwenye viwanja vya Boma wakimsubiri mgombea wa nafasi ya urais kupitia CCM Dkt.John Pombe Magufuli hapo jana.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top