Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

TANGAZO
MAJAMBAZI YAUA MLINZI,YAPORA MILIONI 44 .
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Watu wasiofahamika wamevamia na kumuuua mlinzi wa jadi katika ofisi ya chama cha msingi cha chikundi Amcoss kilichopo katika kijiji cha Mtunungu kata ya Mwena tarafa ya chikundi Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na kufanikiwa kuiba pesa shilingi milioni 44.
Aidha majambazi hayo yalitekeleza unyama huo kwa kuwafunga kamba mikononi na miguuni huku wakiwaweka nguo kwenye vinywa vyao na kuwaziba kwa kutumia plasta mdomoni na puani askari wawili wa jadi waliokuwa wanalinda ofisi hiyo ya chama cha msingi huku mmoja wa walinzi hao akifanikiwa kujiokoa na hatimaye kukimbia.
Mlinzi aliyeuawa kwenye tukio hilo la kinyama ni Valentino Gilbert (70) mkazi wa chikundi na kwamba mlinzi wa pili ambaye alifanikiwa kujiokoa kwa kutumia mbinu za kiaskari kwa maelezo yake huyo alitambuliwa kwa jina la Bakari Ibrahimu (40).
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa 9:30 Alfajiri huko katika kijiji cha Mtunungu kwenye ofisi ya chama cha msingi cha chikundi ambapo kundi la watu wasiofahamika wakiwa na silaha walivamia ofisi hiyo na kuvunja na hatimaye kufanikiwa kuondoka na fedha shilingi milioni 44 mali ya chikundi Amcoss.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara Augustino Ollomi  alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema usiku wa kuamkia leo majira ya saa 9:30 alfajiri kundi hilo la watu wanaosadikiwa kuwa wanne walivamia ofisi hiyo na kumuua mlinzi mmoja huku mlinzi wa pili akifanikiwa kujiokoa.
Alisema majambazi hayo yaliyokuwa na silaha yaliwavamia walinzi hao na kuwafunga kamba miguu na mikono yao huku wakiwaziba midomo yao kwa nguo na kuweka plasta kwenye vinywa vyao pamoja na pua mazingira yaliyopelekea kushindwa kupumua kwa mlinzi huyo mzee na hatimaye kufariki dunia.
Alisema siku ya tukio katibu wa tawi hilo la Chikundi Amcoss Hassani Simkambi pamoja na mjumbe wa bodi ya chama hicho Desteria Sellemani waliondoka ofisini hapo majira ya saa 12:00 jioni baada ya kumaliza zoezi la ugawaji fedha kwa wanachama wao kwa awamu ya kwanza malipo ya pili huku fedha iliyobaki shilingi milioni 44 wakiiacha kwenye mfuko wa sandarusi nyuma ya sanduku la kuhifadhia fedha kinyume na utaratibu.
Ollomi alisema viongozi hao walienda kwa katibu mkuu wa chama hicho Philipo Kambanga kwa ajili ya kupeleka funguo kama ilivyo kawaida ya siku zote lakini kwa mshangao katibu huyo aliwaruhusu funguo hizo waondoke nazo ili wawahi kufungua ofisi siku ya pili asubuhi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo alisema mlinzi Bakari Ibrahimu aliyefanikiwa kujiokoa ndiye aliyeenda kutoa taarifa usiku huo kwa katibu mkuu wa chama hicho na kwamba mara baada ya kupokea taarifa hiyo naye alitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji hicho Clauda Mande majira ya saa 1138 alfajiri na walifanikiwa kufika eneo la tukio na kukuta mlango ukiwa umevunjwa huku mlinzi mmoja akiwa ameuawa fedha imeibiwa.
Alisema polisi walifika kwenye eneo la tukio hilo majra ya saa 3:00 asubuhi na kufanikiwa kufanya mahojiano na wakazi wa maeneo hayo huku wengi wao wakiwa hawaelewi na kwamba wameshtushwa na tukio hilo la mauaji ya mlinzi huyo.
Kufuatia tukio hilo jeshi la polisi mkoa wa Mtwara linawashikila watu wanne kwa mahojiano zaidi wakiwemo mwenyekiti wa chama cha msingi Chikundi Ismail Chilumba,katibu mkuu wa chama hicho Philipo Kambanga,katibu wa tawi la Mtunungu Hassani Simkambi,mjumbe wa bodi Desteria Selemani pamoja na Bakari Ibrahimu ambaye ni mlinzi aliyenusurika kufa.

Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top