Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

WEZI WA VIFAA VYA KOMPYUTA MASHULENI WATANGAZIWA KIHAMA CHAO

TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara Andrew Mtumusha amewaagiza walimu wakuu wa shule za msingi wa kata ya Marika mjini humo yenye shule sita kupeleka majina ofisi ya mkurugenzi ya walimu ambao hawaishi katika vituo vyao vya kazi ili hatua kali za kisheria na kinidhamu  zichukuliwe dhidi yao.

Aidha ametoa onyo kali kwa maofisa watendaji wa vijiji,wenyeviti wa vitongoji pamoja na ofisa mtendaji kata wa kata hiyo ya  Marika Halmashauri ya mji wa Masasi kuwa atakayeshindwa kusimamia agizo hilo ni bora aandike barua mwenyewe kwa mkurugenzi wa mji ya kuacha kazi kabla mkono wa sheria haujamfikia.

Pia amekemea vikali vitendo vya wizi wa vifaa vya kompyuta mpakato vilivyotolewa kama msaada kwenye shule za msingi za Halmashauri hiyo kutoa shirika la maendeleo la Marekani (USAID) kupitia programu ya elimu ya msingi kwa karne ya ishirini na moja-Tz 21 na kwamba watakaobainika watafikishwa mahakamani.

Aliyasema hayo jana wakati wa hafla fupi ya uhamasishaji kusoma vitabu pamoja na majarida mbalimbali  katika shule za msingi mkoani Mtwara hafla iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mumbaka kata ya Marika Halmashauri ya mji wa Masasi na kuratibiwa na Taasisi ya Better Foundation chini ya udhamini wa  Tz 21.

Alisema walimu wengi wa shule za msingi  wa kata hiyo wamekuwa wakiishi nje ya vituo vyao vya kazi kwa kigezo kuwa wako jirani na makao makuu ya Halmashauri hiyo ambapo ameweka wazi msimamo wake kuwa hatokubali kwa mwalimu yeyote ambaye yuko nje ya kituo chake cha kazi aendelee kuishi huko.

Alisema kuwa licha ya uhaba wa nyumba za walimu kwenye baadhi ya shule za msingi za kata hiyo lakini bado nyumba za kupanga zipo kama hizo ambazo wengi wao wamepanga Mjini na kwamba kwa sasa karibu vijiji vyote vya Halmashauri hiyo ziko nyumba bora na za kisasa za watu binafsi ambazo walimu hao wanaweza kupanga na kuishi kama wanavyoishi mjini.

Kwa mujibu wa Mtumusha alisema Halmashauri yake kwa kushirikiana na serikali kuu  iko mbioni kuanza ujenzi wa nyumba za walimu kwenye shule za msingi ambazo tatizo ni kubwa hivyo ametoa rai kwa walimu wakuu wa shule hizo waanze uhamasishaji wa ufyatuaji wa matofali mara baada ya kipindi cha masika kumalizika.

Akizungumzia kuhusu suala la wizi wa vifaa vya kielektroniki vilivyotolewa na USAID kama msaada kwa shule za msingi za Halmashauri hiyo alisema kwa sasa ifike mwisho kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo visivyo vya kiungwana kwa wafadhili hivyo ni vyema jamii ikawa mlinzi wa vifaa hivyo.

“Hatuwezi kupewa msaada wa  vifaa vya kompyuta kwa watoto wetu ili waendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia….halafu kuwe na watu wachache wanaoiba vifaa hivyo huku wananchi mkikaa kimya kwa kuwa hao wanaoiba wengine ni watoto wenu,rafiki zenu na ndugu zenu…hivyo naagiza kwa watendaji wa vijiji kusimamia hilo na atakayeshindwa aache kazi”.alisema.

Akijibu malalamiko yaliyotolewa kwenye risala iliyosomwa na mwanafunzi Martha Alex (8) wa darasa la pili wa shule ya msingi Mumbaka kuhusu wanafunzi wa elimu ya awali  shuleni hapo kusomea kwenye nyumba ya mwalimu,Mtumusha alisema Halmashauri itajenga darasa hilo la awali mara baada ya kipindi cha mvua kumalizika huku akitoa wito kwa wazazi kuchangia ujenzi wa darasa hilo.

Hata hivyo ili kuhamasisha  ujenzi wa darasa hilo mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi aliendesha harambee ndogo iliyokuwa na mafanikio makubwa kwani jumla ya ahadi ya mifuko ya saruji 31,bati tano,boriti 4 pamoja na fedha shilingi 25,000 zote zikiwa ni ahadi zilipatikana.

Mwisho.

 MKURUGENZI wa Better Nation Foundation Hans Gabriel akizungumza wakati wa Hafla fupi iliyokuwa na lengo la kuhamasisha usomaji wa vitabu kwenye viwanja vya shule ya msingi Mumbaka.
 Gari inayobeba vifaa pamoja na wasanii wa kikundi cha Better Nation Foundation kinachotoa burudani yenye lengo la kuhamasisha wananchi umuhimu wa kusoma vitabu.
 Mwanafunzi wa shule ya msingi Mumbaka MARTHA ALEX mwenye umri wa miaka 8 anayesoma darasa la pili shuleni hapo akisoma Risala kwa mgeni rasmi wakati wa sherehe za uzinduzi wa wiki ya uhamasishaji wa kusoma. Mtoto huyo ni matunda ya Programu ya Tz 21 na kwamba malengo yake ni kuja kuwa mwalimu wa shule ya Sekondari hapo baadae.
 WANAFUNZI kutoka kwenye shule mbalimbali za kata ya Marika wakicheza muziki kwa furaha mara baada ya uzinduzi wa zoezi la uhamasishaji wa kusoma katika Halmashauri ya mji wa Masasi Mkonai Mtwara.
 MOJA ya madarasa yanayotumika katika kufundishia kwa kutumia Kompyuta katika shule ya msingi Mumbaka.
 KIKUNDI cha Sanaa cha Better Nation Foundation kikiwaburudisha wananchi pamoja na wanafunzi katika viwanja vya shule ya msingi Mumbaka hapo jana.
 Better Nation wakiwa kwenye burudani ili kutoa hamasa kwa jamii kusoma vitabu
 HUU NI MTI WA VITABU AMBAO WANAFUNZI HUJISOMEA WAKIWA ENEO LA SHULE
MWENYEKITI wa Halmashauri ya mji wa Masasi Andrew Mtumusha akimkabidhi kipaza sauti mratibu elimu kata ya Marika mwalimu Shabani Mkieti ili atoe ahadi kwa wananchi wakati wa zoezi la harambee kuchangia ujenzi wa chumba cha darasa kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya awali.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top