TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Serikali kupitia wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imemwagiza
katibu Tawala mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na mganga mkuu wa mkoa huo
kuhakikisha kiasi cha Shilingi 89
milioni zinapelekwa katika hospitali ya rufaa ngazi ya mkoa ya mtakatifu Benedictine Ndanda .
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika ziara yake hospitalini hapo
Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Stephen Kebwe alisema kiasi hicho cha
fedha ni kati ya Shilingi milioni 178 zilizotoka hazina na kuelekezwa kwenda
katika hospitali hiyo kwa ajili ya mishahara pamoja na mafunzo ya vitendo
lakini zilizofika hospitalini hapo ni Shilingi 89 milioni pekee.
Alisema kiasi cha shilingi milioni 89 kati ya hizo ziliishia
mkoani Mtwara na kwamba uongozi wa mkoa huo ni lazima wahakikishe kuwa fedha
hizo zinapelekwa ili wananchi wanaopata huduma katika hospitali hiyo waweze
kuhudumiwa katika mazingira yaliyo bora.
Aidha waziri huyo wa afya na ustawi wa jamii alitumia ziara hiyo
kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maabara ya kisasa unaoendelea hospitalini
hapo.
Kebwe alisema pesa yoyote inayotoka hazina kwenda popote nchini ni
vyema kabla ya matumizi ziuliziwe ni za kazi gani ili kuepusha kukwama kwa yale
mambo yaliyokusudiwa ikiwemo miradi ya maendeleo.
“Namwagiza katibu tawala na mganga mkuu wa mkoa wahakikishe Shilingi
89 milioni zilizokwama mkoani zinakuja Ndanda kama ilivyokusudiwa ili ziweze
kutumika mahali ambapo serikali ilipanga fedha hizo zitumike”.alisema Kebwe.
Alisema Wizara kwa kushirikiana
na shirika la afya ulimwenguni (WHO) liliona kuna umuhimu wa kuboresha huduma za
maabara nchini ili ziweze kutoa huduma bora na za uhakika katika kiwango cha
kimataifa hivyo ni imani ya serikali kuwa
kukamilika kwa maabara hiyo kutaondoa utaratibu wa kwenda kupima sampuli za magonjwa
kama ebola nje ya nchi.
Awali akisoma risala kwa waziri daktari bingwa wa magonjwa na afya
ya watoto, Stanslaus Wambyakale alisema kuwa hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa
na uhaba wa fedha za kulipa watumishi, wodi ya watoto wachanga, gari ya kubeba
wagonjwa pamoja na watumishi.
Alisema hospitali hiyo ni moja ya hospitali mkoani Mtwara
inayohudumia wagonjwa kutoka sehemu mbalimbali za mikoa ya kusini pamoja na nchi
jirani ya Msumbiji hivyo wameiomba serikali kuitilia mkazo hospitali hiyo.
Akizungumza mmoja wa wazazi aliyekuwa katika wodi ya watoto
hospitalini hapo, Amina Hamis alisema kuwa wamekuwa wakipatiwa huduma kwa wakati
pindi wanapofika hospitalini hapo lakini changamoto wanayokumbana nayo ni
msongamano wa wagonjwa.
Alisema huduma zitolewazo na hospitali hiyo ni nzuri na kwamba
wamekuwa wakilipia michango kidogo tofauti na hospitali zingine kwani wamekuwa
wakichangia shilingi 10,000 tu kwa wanaojifungua kwa njia ya kawaida huku wale
wanaofanyiwa upasuaji wakichangia shilingi 25,000.
Maabara inayojengwa katika hospitali ya Misheni ya Ndanda mkoani
Mtwara ni miongoni mwa maabara saba zilizoteuliwa nchini kwa kufuata vigezo
vilivyowekwa na wataalamu wa afya kuingia katika mradi huo.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD