TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya mji WA Masasi Mkoani Mtwara, Fortunatus Kagoro amewataka
wananchi mjini humo kuwa na moyo wa uzalendo na mji wao katika kuchangia ujenzi
wa maabara za shule za sekondari zilizopo kwenye Halmashauri hiyo.
Pia amemuomba
mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi Andrew Mtumusha kuwashawishi
madiwani wa halmashauri hiyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maabara.
Alitoa kauli hiyo
jana wakati wa hafla fupi ya wadau wa maendeleo ya elimu iliyokuwa na lengo la
kuchangia ujenzi wa maabara ili kuendana na agizo la Rais iliyofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano katika shule ya sekondari ya
wasichana Masasi.
Alisema ni vyema kila
mwana jamii wa mji wa Masasi akaona umuhimu wa kuchangia ujenzi wa maabara hizo
ambazo ni watoto wa Masasi ndio watakaosoma ili baadae waje wafanye kazi katika
viwanda vya gesi iliyogundulika mkoani Mtwara.
Kwa mujibu wa Kagoro
alisema Halmashauri inayo jukumu la kufanya kwa nafasi yake lakini pia jamii
kwa ujumla nayo ina nafasi yake katika kushiriki kwenye ujenzi wa maabara hizo
zenye lengo la kupata wataalamu wa masomo ya sayansi.
“Maabara hizi
tunazozijenga ni kwa ajili ya watoto wa Masasi…ambao hapo baadae watakuja kuwa
madaktari na walimu wazuri wa masomo ya sayansi,hivyo jamii ni wajibu wenu
kuchangia ujenzi wa maabara hizo”.alisema Kagoro.
Alisema kupitia
madiwani ambao ndio wawakilishi wa kata ambamo maabara hizo zinajengwa wananchi
waelimishwe na waombwe wawe na moyo wa kujitolea kwa kutumia nguvu kazi zao na
wakatio mwingine hata michango ya fedha ama vifaa vya ujenzi.
Mkurugenzi huyo
aliongeza kwa kusema kuwa kwa sasa nchini kumekuwa na ushindani mkubwa wa elimu
mazingira yanayopelekea nafasi za ajira kuwa chache na zenye ushindani hivyo
watoto wa Masasi wakisoma Masomo ya sayansi watakuwa ni miongoni mwa washindani
wakubwa katika soko la ajira.
“Wakati Fulani
nilitembelea mkoa wa Njombe nilifika kwenye nyumba ya kulala wageni…lakini
katika hali ya kushangaza nilikuta tangazo la nafasi za kazi mlangoni
wakihitaji mchinja kuku kwa masharti ya kuwa ni lazima awe amefikia kidato cha
nne”.alisema.
Alisema suala la
ujenzi wa maabara ni muhimu ambalo linahitaji msukumo mkubwa na kwamba kwa
vyovote itakavyokuwa Halmashauri yake itajitahidi kukamilisha ujenzi wa maabara
hizo.
Katika hafla hiyo
iliyohudhuriwa na wageni mbalimbali jumla ya fedha shilingi milioni 90
zilihaidiwa kutoka kwa wadau wa maendeleo wa mji wa Masasi huku mahitaji yakiwa
ni shilingi milioni 140.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD