Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

WANAFUNZI WA KIKE WA SEKONDARI WANAPASWA KUENDELEA NA MASOMO HATA BAADA YA KUPATA MIMBA.

TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Jumla ya wanafunzi 50 kutoka kwenye shule 10 za sekondari zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Masasi mkoani Mtwara wameshiriki kwenye mdahalo mkubwa wa kielimu uliokuwa na lengo la kujadili masuala yahusuyo taaluma uliofanyika kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Masasi.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa mdahalo huo Ofisa elimu taaluma kwa shule za sekondari wa Halmashauri ya mji wa Masasi Upendo Rweyemamu alisema midahalo hiyo ni miongoni mwa  mipango mkakati ya idara ya sekondari katika kukuza stadi ya uzungumzaji wa lugha ya kiingereza ambayo imekuwa changamoto kwa wanafunzi wengi nchini.

Alisema baadhi ya wanafunzi wa sekondari wamekuwa wakifanya vibaya mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne kutokana na kutoifahamu kwa ufasaha lugha ya kiingereza ambayo ni lugha inayotumika katika ufundishaji wa masomo yote katika shule za sekondari ukiondoa Kiswahili pekee.

Kwa mujibu wa Rweyemamu alisema kuwepo kwa mpango huo wenye manufaa kwa wanafunzi pamoja na Halmashauri kwa ujumla kunatokana na mshikamano uliopo kati ya idara ya elimu ya sekondari,walimu wakuu wa shule hizo pamoja na walimu wao ambao wamekuwa na msukumo mkubwa kwa wanafunzi kuweza kushiriki midahalo mbalimbali inayoandaliwa.

“Wanafunzi mnachotakiwa kujua ni kuwa hamko hapa kupoteza muda kwa kuwepo na kushiriki kwenye mjadala huu wa leo…kuwepo kwenu hapa kutasaidi nyinyi wenyewe kuongeza uelewa katika kuzungumza lugha ya kiingereza na nawaomba mjiamini,msiwe na hofu pale mtakapopata nafasi ya kuchangia mjadala huu”,alisema Rweyemamu.

Aidha Rweyemamu alitumia nafasi hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wakuu wa shule pamoja na walimu wote wa shule hizo hasa wale wanaofundisha masomo ya kiingereza kwa jitihada kubwa wanazozifanya kwenye shule zao ambazo matunda yake yameanza kuonekana kwa baadhi ya wanafunzi kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kidato cha nne.

Katika mdahalo huo mada kuu iliyojadiliwa ni “wanafunzi wa kike wa sekondari wanapaswa kuendelea na masomo hata baada ya kupata ujauzito” mada iliyoibua hisia na mvutano mkali kwa kundi lililokuwa linaunga mkono hoja na lile lililokuwa linapinga hoja huku makundi yote yakionekana kutoa michango yenye tija kwa mwanafunzi wa kike.

Kwa upande wake mratibu wa mdahalo huo mwalimu Humud Mpende mkuu wa shule ya sekondari ya Mtandi alisema jitihada zinazofanywa na walimu wa shule za sekondari Halmashauri ya mji wa Masasi zinapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa elimu na halmashauri kwa ujumla.
WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI YA MTANDI
Alisema midahalo hiyo ni mwendelezo ambao tangia mwaka jana wamekuwa wakifanya midahalo hiyo mara kwa mara ili kukuza stadi za kuzungumza lugha ya kiingereza sambamba na kumpa mwanafunzi uwezo wa kujiamini na namna ya kuwasilisha mada mbele ya hadhira.

Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top