TANGAZO
![]() |
Sheikh Nurdin Abdallah Mangochi |
Na Fatuma Maumba,Mtwara.
WATANZANIA wametakiwa
kuendeleza na kudumisha amani, upendo, mshikamano na umoja waliokuwepo nao
miaka yote, hasa kipindi hiki Taifa linapoelekea kwenye mchakato mzima wa kura
za maoni pamoja na Uchaguzi Mkuu unawajumuisha Madiwani,Wabunge, na Rais.
Ushauri huo umetolewa hivi karibuni, mjini
hapa na Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Sheikh Nurdini Mangochi, wakati akiongea
na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa
BAKWATA mkoa.
Alisema suala la amani,upendo ,
mshikamano umoja si la Serikali tu, hata mtu mwenyewe akiwa nyumbani kwake
anatakiwa awe na amani na upendo na familia yake.
“Suala la amani, upendo,
mshikamano na umoja si suala la Serikali pekee hata wewe mwenyewe unapokuwa
nyumbani kwako unatakiwa uwe na amani na upendo na familia yako…kwa hiyo mimi
naomba watu wote Tanzania Nzima ambao watagombea nafasi ya Udiwani,
Urais na Ubunge basi watangulize mbele amani ndio msingi wa maisha kwani kama
hakuna amani shughuli zote zinasimama na watu hawatafanya kazi kwa uhuru, kama
kiongozi wa dini basi nasisitiza amani itawale siku zote katika maisha yetu.
Pamoja na mambo mengine Sheikh
Mangochi, alisema kwamba kiongozi yoyote hapa duniani kitu cha
kwanza anachotakiwa afanye ni kusimamia na kuzingatia maadili ya kazi yake
ndipo ataendesha vizuri uongozi wake.
Alisema kuwa sehemu yeyote ile ya
kazi ukisikia kuna migogoro basi kiongozi amekiuka maadili ya kazi yake, kwa
hiyo ni vizuri viongozi wakafuata maadili ya kazi zao ili kuepusha migogoro
isiyokuwa ya lazima sehemu za kazi.
“Tendo la maadili hilo ndio kubwa
sehemu ya kazi, ukisikia kelele nyingi kwenye maofisi basi ujue kuna
kiongozi amekosa maadili, hata nyinyi waandishi wa habari mkikosea
maadili ya kazi yenu tu basi mtasikia watu wanawalalamikia…kwa hili hata mimi
namuomba Mwenyezi Mungu anipe uwezo mzuri nisimamie maadili katika
huu uongozi wangu.
Kwa upande wake aliyekuwa Mwanyekiti
wa Baraza Kuu la Waislamu mkoa wa Mtwara, Alhaji Marijani Dadi, alisema kwamba
katika miaka yake kumi ya uongozi wa Baraza hilo, Waislamu wote wa
mkoa wa Mtwara walikuwa kitu kimoja, na amewataka waendeleze mshikamano huo
uliokuwepo tokea mwanzo.
“Nimekaa madarakani kwa miaka kumi na
katika kipindi chote hicho Waislamu wa Mtwara tulikuwa kitu kimoja na wilaya
zake zote sita hakuna tatizo lolote, leo nakabidhi na husia wangu mkubwa kwa ninaowakabidhi
waendeleze mshikamano wilaya zote ziwe kitu kimoja isiwe watu wa sehemu fulani
wanawatenga wengine,” alisema Alhaji Dadi na kuongeza:
“Vile vile tuzingatie maendeleo ya
nchi yetu kwa sababu kuna michakato mbalimbali sisi kama raia wa nchi hii tuna
haki ya kushiriki, kwa mfano sasa hivi kuna mambo ya Katiba lazima na wao
wasimamie waone kwamba Katiba inafanikiwa kwa maana watu wajitokeze kwenda
kupiga kura zao ili kutoa maoni yao… Kikubwa ninachohimiza ni kwamba
utulivu hauji bure bure kwani wanaodumisha utulivu ni wananchi
wenyewe na sisi ni sehemu katika raia wa nchi hii ni lazima tuhakikishe
tunatimiza wajibu wetu ili utulivu na amani si kwa Mtwara tu basi uambukize na
sehemu nyingine.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD