TANGAZO
Mwaka ambao Hospitali Hiyo imejengwa. |
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Hospitali ya
Mkomaindo iliyopo Halmashauri ya MJi wa Masasi mkoani Mtwara imeiomba serikali
kuisaidia katika ukarabati pamoja na ujenzi wa baadhi ya miundo mbinu iliyopo
hospitalini hapo ili iweze kutoa huduma bora na za kisasa kwa wagonjwa
wanaopata huduma katika hospitali hiyo.
Akizungumza na gazeti
hili Kaimu mganga mkuu wa Hospitali ya Mkomaindo Dkt.Albano Nditi alisema
miundo mbinu mingi ya hospitali hiyo ni chakavu ambayo inahitaji ukarabati
kutokana na baadhi ya majengo hayo yaliyojengwa mwaka 1951 kuonekana muda wake
umepita huku baadhi ya majengo
yakihitaji kujengwa upya.
Alisema hali ya
majengo yaliyopo ya kutolea huduma katika Hospitali hiyo hayaridhishi kwa kuwa
mengi ni ya zamani na yamechakaa na kwamba wanaiomba serikali kusaidia katika
kufanya ukarabati wa majengo hayo likiwemo jengo la utawala lililojengwa na
wakoloni wa kijerumani.
Kwa mujibu wa kaimu
mganga mkuu huyo alisema hospitali hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa majengo hususani
ya kisasa kwa ajili ya kulaza wagonjwa likiwemo jengo la wodi ya kisasa,wodi ya
wagonjwa wa dharura,jengo la kulaza wagonjwa wenye milipuko pamoja na jengo la
kisasa la kuchomea taka.
Alisema licha ya
kupokea msaada wa gari moja la kubebea wagonjwa kutoka kwa mwenyekiti wa
taasisi ya maendeleo ya wanawake nchini (WAMA) Mama Salma Kikwete bado hospitali hiyo inayohudumia wagonjwa wengi
wakiwemo wale wa nchi jirani ya Msumbiji ina uhaba mkubwa wa magari kwa ajili
ya uendeshaji wa shughuli za huduma za afya katika hospitali hiyo.
Alisema kuwa kwa sasa
hospitali hiyo ina magari mawili tu ambayo yote ni ya kubebea wagonjwa huku magari mengine mawili yakiwa hayafanyi
kazi kutokana na ubovu ambao unahitaji matengenezo makubwa ama kubadilishwa kwa
magari hayo na kwamba hali ya utendaji kazi hospitalini hapo imekuwa ya
kusuasua kutokana na kukosekana kwa usafiri wa uhakika kwa wafanyakazi.
Dkt.Nditi alieleza
kuwa kutokana na uhaba wa magari wafanyakazi wa hospitali hiyo wanalazimika
kutumia magari ya kubebea wagonjwa kufanya safari mbalimbali za kikazi kitu
ambacho amekiri kuwa ni kinyume na maagizo ya wizara ambapo amesisitiza kuwa
bado kilio chao wanakilekeza kwa serikali iweze kutatua changamoto hizo.
Alizitaja changamoto nyingine
kuwa ni pamoja na kukosekana kwa gari kubwa kwa ajili ya kusafirishia mizigo
mbalimbali pamoja na kuhamisha watumishi wa idara hiyo kutokana na gari aina ya
Isuzu tani saba lililokuwepo kuchomwa moto wakati wa vurugu zilizotokea januari
2013.
Aidha Changamoto
zingine alizozibainisha ni uchache wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa kutoka
bohari kuu ya madawa (MSD) zinazotolewa na wizara ya afya hivyo kusababisha
uhaba wa dawa,ukosefu wa majokofu ya kuhifadhia chanjo kwa ajili ya huduma za
afya ya uzazi na mtoto,pamoja na idadi ndogo iliyopo ya watumishi mazingira
yanayopelekea huduma kutotolewa kwa wakati.
Akizungumza kuhusu
mikakati iliyopo kwa ajili ya kukabiliana na baadhi ya changamoto hizo kaimu mganga mkuu huyo alisema
idara inaendelea kuomba watumishi kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii
pamoja na kununua vitanda na shuka kwa awamu pindi fedha itakapopatikana.
Kwa upande wake
mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Masasi ambaye pia ni diwani wa kata ya
Nyasa Andrew Mtumusha alisema Halmashauri itaendelea kufanya ukarabati wa
baadhi ya majengo chakavu katika hospitali hiyo pamoja na yale yaliyopo katika
vituo vya afya na zahanati kutegemea na upatikanaji wa fedha kutoka kwenye mapato
yake ya ndani licha ya kuendelea kuiomba serikali kutoa kipaumbele katika
hospitali hiyo kongwe nchini.
Idara ya afya
Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara ina vituo 13 vya kutolea huduma za
afya ikwemo hospitali moja ya Mkomaindo,Kituo kimoja cha afya,zahanati 11 huku
kwa upande wa watumishi idara hiyo ina madaktari watano tu huku mahitaji yakiwa
ni madaktari 25 ambapo pungufu ni madaktari 20.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD