TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Mtwara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora Kapteni Mstaafu George
Mkuchika amesema kwa sasa hali ilivyo Manispaa ya Mtwara Mikindani ina kila
sababu ya kupewa hadhi ya kuwa Jiji kutokana na kukidhi vigezo ikiwemo ongezeko
kubwa la watu Mkoani humo.
Pia alisema kugundulika kwa gesi asilia kunakopelekea kujengwa kwa
viwanda vingi ni miongoni mwa sifa ambazo ni dhahiri Manispaa hiyo kwa sasa ina
sifa ya kuwa jiji huku akimuomba mkuu wa mkoa huo Halima Dendego kupeleka kilio
chao wana Mtwara kwa Rais Jakaya Kikwete ili kabla ya kumaliza awamu yake awape
Mtwara kuwa Halmashauri ya Jiji.
Mkuchika aliyasema hayo juzi wakati wa tafrija ya usiku wa
mwanamke iliyoenda sambamba na zoezi la kukaribisha na kuwaaga viongozi wa mkoa
wa Mtwara akiwemo aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia
pamoja na wakuu wa wilaya katika ukumbi
wa Makonde Beach Resort.
Alisema mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa mikubwa nchini hivyo
ni vyema serikali iliyo chini ya chama cha CCM ikaona uwezekano wa kuipa hadhi
ya kuwa jiji ili kuendana na kasi iliyopo hivi sasa mkoani humo ambapo
amewataka wana Mtwara kumuunga mkono katika jitihada hizo za kuifanya Manispaa
ya Mtwara kuwa jiji.
Kwa mujibu wa Mkuchika alisema mkoa wa Mtwara ni mkoa wa Chama
Tawala cha CCM na hilo limejidhihirisha wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa
ambao chama hicho kimefanya vizuri katika maeneo mengi mkoani Mtwara na kwamba
kwa yale maeneo ambayo wamefanya vibaya watahakikisha uchaguzi ujao wanashinda.
“Mimi na umri wangu huu wa uzee wa miaka 67 kamwe sitakubali siku moja kushuhudia ndani ya mkoa wa Mtwara
akiapishwa mbunge wa chama cha upinzani…hivyo ni vyema wana Mtwara tuungane na
tuichague CCM ili tupate maendeleo ambayo kwa sasa yameanza kuonekana”.alisema.
Aidha Mkuchika alielezea kufurahishwa kwake na uteuzi wa Rais
Kikwete wa kumteua Halima Dendego kuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara kwani ni mtu
mchapakazi,mwadilifu na asiye na majungu na kwamba wao wana Mtwara wamepokea
kwa mikono miwili uteuzi huo.
Alisema wananchi wa mkoa wa Mtwara ni wapenda maendeleo huku
matarajio yao kwake yakiwa ni makubwa katika kipindi chake cha uongozi mkoani
humo ambapo amemuomba ajitahidi kusimamia elimu kwa kuwa historia inaonesha
kuwa mikoa hiyo ilichelewa kupata elimu kutokana na serikali kuifanya kuwa ni
mikoa ya kambi za kijeshi wakati wa mapigano ya nchi jirani za Msumbiji,Afrika
ya kusini na niynginezo.
Mkuchika alisema matarajio yao mengine ni kuona kuwa Hospitali ya
mkoa ya Ligula inapewa hadi ya kuwa hospitali ya rufaa ya kanda,Halmashauri
zote mkoani humo zikeendelea kupata hati safi kama ilivyo sasa pamoja na
kuimarishwa kwa kuwekwa kiwango cha lami katika barabara ya kiuchumi itokayo
Mtwara kuelekea Nanyamba
-Tandahimba-Newala hadi wilayani Masasi.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego alimuhakikishia
waziri Mkuchika kuwa kwa kutumia elimu yake,uzoefu wake kazini pamoja na
uanachama wake wa CCM kuwa atasimamia shughuli zote za maendeleo zilizopangwa
mkoani humo kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya wa wilaya zote za mkoa huo.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD