TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Ruangwa.
Naibu waziri wa Maji
Amosi Makala amewahakikishia wananchi
wa kijiji cha Chinongwe wilayani Ruangwa
katika mkoa wa Lindi kuwa serikali kupitia wizara ya maji imesikia kilio chao
cha muda mrefu kuhusu fidia kutokana na zoezi la usambazaji wa maji kupitia
mradi mkubwa wa Mbwinji na kwamba tayari fedha za fidia hizo zimeshapatikana.
Alitoa kauli hiyo ya
furaha kwa wananchi hao jana wakati anawahutubia maelfu ya wakazi wa kijiji cha
Chinongwe na vijiji jirani wakati wa ziara yake yenye lengo la kutembelea pamoja
na kukagua miradi ya Maji nchini
inayotekelezwa na serikali.
Alisema serikali
kupitia wizara ya maji tayari imeshatoa fedha shilingi milioni 85 kwa ajili ya
kulipa fidia kwa wananchi ambao tathimini ilishafanyika hapo awali na kwamba
vijiji vilivyonufaika na malipo ya fidia hiyo ni pamoja na
Chinongwe,Chiumbati-Miembeni,Likwachu pamoja na Tunduru ya leo.
Makala alisema
wananchi wasubiri taratibu za malipo yao kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya ya
Ruangwa ambapo amewahaidi kuwa hakuna mtu yeyote ambaye yupo kwenye orodha ya
majina yaliyohakikiwa atakosa kulipwa fidia hiyo.
Aidha katika hotuba
yake alimpongeza mbunge wa jimbo la Ruangwa Kassimu Majaliwa kwa jitihada
alizozifanya za kusukuma malipo ya deni hilo la fidia kwa wakazi wa vijiji
hivyo ambapo amewaomba wananchi hao waendelee kumuunga mkono mbunge huyo katika
shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Ndugu zangu kiukweli
mnaye mbunge mahiri anayechapa kazi kwa bidii katika kuhakikisha kuwa kila
mwananchi anapata huduma bora pamoja na maslahi yake binafsi…na ushahidi ni hii
leo ambapo huyo huyo mbunge wenu amefuatilia sana madai yenu na hatimaye hii
leo fedha yenu imepatikana na imetumwa ofisi za maji mkoani Mtwara”.alisema.
Alisema wananchi
wapuuze maneno yanayotolewa na baadhi ya watu wakidai kuwa serikali imekuwa haijali
matatizo ya wananchi na kwamba huo ni uzushi usio na maana hasa Taifa
likielekea kwenye mambo ya msingi ikiwemo maoni ya katiba
inayopendekezwa,daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na uchaguzi mkuu oktoba
mwaka huu.
Mwisho.
Naibu waziri wa Maji ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mvomero Amosi Makala aliyevaa shati la kitenge akiwa na mwenyeji wake mkuu wa wilaya ya Masasi Bernald Nduta mwenye suti alipowasili kwenye ofisi za mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Masasi-Nachingwea(MANAWASA) wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD