TANGAZO
![]() |
Mbunge wa Jimbo la Ruangwa Kassimu Majaliwa. |
Na
Mwandishi wetu, Ruangwa.
Wazazi na walezi wa watoto wanaosoma
kwenye Shule ya Msingi ya Mnacho katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi
wametakiwa kuhakikisha kuwa watoto wao wanahudhuria masomo yao na wanapaswa
kufuatilia maendeleo yao kitaaluma kwa watoto wao.
Wito huo umetolewa shuleni hapo Jana
na Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya maendeleo ya wanawake Mama Salma Kikwete
kwenye sherehe ya kukabidhi madawati 100 ambapo amewahimiza
wazazi hao kuthamini elimu ya watoto kwani ndio tunu bora kwa maisha ya baadaye
ya watoto wao.
Alisema, akiwa Mwalimu Mwanafunzi alianza kufundisha
kwenye shule hiyo na Februari mwaka jana alitembelea shule hiyo na kukuta upungufu wa madawati mazingira
yaliyomfanya atoe Milioni 5 na kumkabidhi Mbunge wa Jimbo la
Ruangwa,Kasim Majaliwa ili anunue madawati
hayo aliyoyakabidhi.
Akizungumzia juu ya uchaguzi Mkuu ujao
Mama Kikwete aliwahamasisha wakazi wa Vijiji vya Tarafa ya Mnacho waliohudhuria
sherehe hiyo fupi kuendelea kumpa kura Mbunge Majaliwa kusudi awaletee maendeleo
yao katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Kama Rais amemchagua kuwa Naibu
Waziri Tamisemi anayeshughulikia Elimu,ni kitu gani kitawafanya ninyi mshindwe
kumchagua Majaliwa kwenye uchaguzi ujao”,aliuliza Mama Kikwete.
Akiyapokea madawati hayo kwa niaba ya
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa,Katibu Tawala,Salvius Kilowoko alimshukuru Mama
Kikwete kwa msaada huo ambao utaongeza ari ya wanafunzi kujifunza kutokana na
uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia.
Baada ya Kilowoko kuyapokea madawati
hayo alimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Nikolaus
Kombe ambaye alisema “Kwa niaba ya Halmashauri yetu napenda kumshukuru Mke wa
Rais kwa kutupatia madawati na nitahakikisha yanatumika kwenye shule hii ya
Mnacho na yanatunzwa ipasavyo”
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la
Ruangwa Kassimu Majaliwa alimshukuru Mama Kikwete kwa kutimiza ahadi aliyoitoa
mwaka jana kwenye shule ambayo yeye alisoma elimu yake ya msingi miaka kadhaa
iliyopita, na kumwomba azifikishe kwa Rais Kikwete salamu za matashi mema
kutoka kwa Wana-Mnacho.
Kwenye Risala ya Shule hiyo ambayo
haikusomwa,Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Stephen Ngondo amezitaja changamoto za
shule hiyo kama vile,mahitaji ya Madawati 45 na ukosefu wa nyumba za
Walimu,kwani kati ya walimu 10 wa Mnacho wenye nyumba ni wawili tu, huku
wengine wanane wakiishi nyumba za kupanga.
Changamoto nyingine ni uchakavu wa
majengo kwa kuwa yaliyopo yamerithiwa toka kwa Wamisionari wa Kanisa Katoliki
waliojenga majengo hayo mwaka 1932 kabla Serikali haijataifisha mwaka 1963.
Kwa upande wa taaluma shule hiyo yenye
wanafunzi wapatao 371 wakiwemo wavulana 177 na wasichana 194 ina ukosefu pia wa
vitendea kazi kama vile vivunge vya Sayansi, Hisabati pamoja Jiografia
unaosababishwa na ruzuku ndogo inayoletwa shuleni hapo.
Sherehe hiyo ilihitimishwa na utoaji
wa zawadi ambapo wazazi na walezi ambao watoto wao wanasoma kwenye shule hiyo
walimkabidhi Mama Kikwete dume la mbuzi.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD