TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Hospitali ya Mkomaindo iliyopo Halmashauri ya Mji wa Masasi
imepewa msaada wa vifaa mbalimbali vitakavyotumika hospitalini hapo kwa
wagonjwa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara.
Vifaa vilivyokabidhiwa kwa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo
Dkt.Musa Rashidi ni pamoja na mashuka 85,chandarua 55 na ndoo kubwa tano vyote
vikiwa na malengo ya kuboresha usafi sambamba na kulinda afya za akinamama na
watoto.
Akikabidhi msaada huo jana kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa
Mtwara,Mganga mkuu wa mkoa wa Mtwara Dkt.Shaibu Maarifa alisema vifaa hivyo ni
sehemu ya vifaa vilivyopatikana kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo
waliochangia wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
yaliyofanyika kwenye viwanja vya mashujaa mkoani Mtwara.
Alisema Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego aliamua kuvigawa
vifaa hivyo kwa baadhi ya hospitali zilizopo mkoani humo mkomaindo ikiwemo ili
kupunguza za changamoto za upungufu wa vifaa zinazozikabili hospitali hizo
mkoani humo.
Kwa mujibu wa mganga mkuu huyo alisema kupatikana kwa vifaa hivyo
ni ukombozi kwa hospitali hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa na uhaba wa
vifaa hivyo hasa mashuka huku akitoa wito kwa wadau wengine mkoani humo kuunga
mkono jitihada zinazofanywa na mkuu wa mkoa huo katika kutoa michango
mbalimbali kwenye jamii.
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa hospitali ya Mkomaindo
Dkt.Mussa Rashidi alisema wanaishukuru ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara kwa
kuwapa msaada huo ambao umefika kwa wakati muafaka kutokana na adha waliyokuwa
nayo ya upungufu wa vifaa katika hospitali hiyo.
Alisema licha ya kupokea msaada huo lakini bado wanakabiliwa na
changamoto kubwa ya vifaa vikiwemo vitanda kwa ajili ya wagonjwa, uchakavu wa
majengo ambayo yamejengwa tangu mwaka 1951 wakati wa ukoloni ambayo kwa sasa
hayana hadhi ya kuwa hospitali ya wilaya.
Alisema bado wana upungufu mkubwa wa mashuka licha ya kupewa hayo
85 kwa kuwa mahitaji ni 2050 yaliyopo ni 300 huku upungufu ikiwa ni mashuka
1750 ambapo wamemuomba mkuu wa mkoa kuendelea kuwasaidia katika kuchangia vifaa
katika hospitali hiyo pindi vinapopatikana.
Kwa mujibu wa Dkt.Mussa alisema hali si ya kuridhisha katika
hospitali hiyo kwani kitaalamu kila kitanda kimoja cha mgonjwa kinahitajika
kuwepo na shuka nane na kwamba kwa sasa uwezo wao kila kitanda kina shuka mbili
tu mazingira ambayo ni hatari kwa afya za wagonjwa wanaolazwa katika hospitali
hiyo.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD