TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Lindi.
Naibu Waziri wa kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, amesema kuwa
hali ya ukosefu wa ajira nchini mpaka hivi sasa kwa mujibu wa utafiti wa nguvu
kazi uliofanyika mwaka 2006, jumla ya watu waliokuwa hawana kazi hapa nchini ni
asilimia 11.7.
Aliyasema hayo juzi wakati wa ufunguzi wa semina ya vijana mkoa wa Lindi
ambapo alisema utafiti huo ulionesha
kuwa takribani asilimia 13.4 ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 34 wa
Tanzania hawana kazi kabisa.
Alisema tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ni kubwa zaidi
maeneo ya mijini kwa asilimia 26.7
ukilinganisha na vijijini asilimia 7.9 na kwamba hali ya ukosefu wa ajira imechangiwa na kiasi
kikubwa na kutofikiwa kikamilifu kwa malengo ya nchi ya kuinua uchumi katika
sekta za kilimo, uzalishaji na viwanda.
Kwa mujibu wa Mahanga alisema vijana wengi wamekuwa na utamaduni wa kukimbilia
mijini na hivyo kupunguza uzalishaji na tija kwenye sekta ya kilimo, lakini pia
kuchangia ongezeko la ukosefu wa ajira mijini sambamba na ongezeko la wafanya
biashara wa sekta isiyo rasmi maarufu kwa jina la machinga.
Aidha alisema kuendelea kupanuka kwa sekta isiyo rasmi kutoka
asilimia 8.8 mwaka 1990/1991 hadi asilimia 11.3 mwaka 2005 na kupungua kwa
nguvu kazi katika sekta ya kilimo kutoka asilimia 83.7 hadi asilimia 74.6 ni
dalili kuwa kuna uhamaji mkubwa wa nguvu kazi kutoka vijijini kwenda mijini.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Mwantumu Mahiza, alisema
kuwa lengo la semina hiyo ni kuwawezesha vijana hao kupata ufahamu na uelewa wa
nafasi yao katika jamii, wajibu wa kijana, haki zake na kuwajengea uwezo ambapo
watapata stadi za namna ya kutambua fursa zilizowazunguka, upatikanaji wa
mahitaji na kujiunga katika mifuko ya hifadhi na Bima ya Afya.
Mahiza alisema, katika semina hiyo ya siku tano, vijana watapata
fursa ya kupitishwa katika mambo mbalimbali, ambapo viongozi kadhaa wameombwa
kutoa mada kama vile mapambano dhidi ya rushwa, usalama wa raia na mali zao,
Katiba inayopendekezwa na ushiriki wa vijana katika kukuza uchumi.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD