Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

TAMKO LA TUME YA HAKI ZA BINADAMU KULAANI MAUAJI YA MTOTO YOHANA BAHATI-MLEMAVU WA NGOZI

TANGAZO










TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tamko la THBUB kulaani mauaji ya Mtoto Yohana Bahati


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na mauaji ya kikatili ya mtoto Yohana Bahati aliyetekwa nyara hivi karibuni katika kijiji cha Ilelema, Chato Mkoani Geita.

Pia Tume inalaani kuumizwa kwa mama yake, Ester Jonas wakati anatetea uhai wa mwanae wakati wa tukio lililotokea Februari 15, 2015.

Tume inapenda kuwakumbusha wananchi kwa ujumla kuwa vitendo vya ukatili wanaofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi, ni matukio ya ukiukwaji wa Sheria na haki za kibinadamu. Matukio haya yanaonesha yamekuwa yakichagizwa na imani za kishirikina hivyo Tume inakemea matendo haya na kutaka yapigwe vita.

Chini ya Katiba na Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu Serikali inao wajibu wa kulinda raia wake. Tume inaiomba Serikali kuwatafuta wale wote wanaohusika na vitendo hivi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya Sheria.

Aidha, Tume inaungana na wananchi, wadau mbalimbali na Serikali kulaani vikali mauaji ya mtoto Yohana Bahati na kujeruhiwa vibaya mama yake wakati akitetea haki ya mwanae kuishi katika jamii huru, na inakemea vikali vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa ujumla.

Tume inaikumbusha Serikali kuwa wakati umefika wa kufanyia marekebisho makubwa Sheria ya Uchawi (Sura ya 18 ya 1928) au kutunga Sheria mpya ili kupiga marufuku vitendo vyote vinavyoendeleza imani za uchawi na ushirikina.

Tume inashauri pia Serikali kupitia upya Sheria inayowatambua waganga wa jadi (Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala).

Tume inatoa wito kwa wananchi na jamii yote kwa ujumla kuachana na imani potofu zenye mtizamo hasi kwamba mafanikio yoyote yanaweza kupatikana kwa njia za kishirikina. Tume inakumbusha wananchi kuwa mafanikio yoyote yatapatikana kwa kufanya kazi zote halali kwa bidii, na siyo kwa njia za kishirikina ikiwemo kutumia viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Tume inaungana na wananchi na Serikali kupiga vita vitendo hivi vya kikatili.

Pia Tume inatoa pole kwa mama aliyeumizwa akitetea uhai wa marehemu mwanae.

Mwisho, Tume iko mbioni kwa kushirikiana na wadau wengine kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuelimisha wananchi ili kuepusha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini. Tume inaomba wananchi wote kushirikiana katika jukumu hili.

Imetolewa na:

 Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Februari 19, 2015


TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top