TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi
Halmashauri ya mji wa masasi ni miongoni mwa
Halmashauri saba zinazounda mkoa wa mtwara ambayo imekuwa ikikua kwa kasi kutokana na kuwa na utajiri wa zao la korosho
linaloifanya Halmashauri hiyo kutamba kuwa imefanikiwa katika sekta ya
uwekezaji na ukombozi wa maisha ya wananchi wake waweze kuwa na maisha bora.
Mji wa masasi pia umejipanga kutumia fursa za
wahisani kutoka ndani na nje ya nchi katika kujenga na kuimarisha miundombinu
mbalimbali na kwa maeneo yote ya barabara, kilimo, mipangomiji, afya, elimu,michezo,uboreshaji
wa mazingira pamoja na maji.
Katika jitihada zake za kuboresha miundo mbinu
yake Halmashauri ya mji wa Masasi imekuwa na ushirikiano wa kirafiki pamoja na
Halmashauri ya wilaya ya Enzkreis ya nchini ujerumani ushirikiano
ulioanza mnamo mwaka 2011 hadi sasa.
Hata hivyo Halmashauri ya mji wa Masasi kupitia
idara ya ardhi imekuwa na mikakati ya uendelezaji mji wa masasi kwa lengo la
kuufanya mji huo uwe miongoni mwa miji hapa nchini yenye sura ya kuvutia kwa
wageni mbalimbali wanaokuja kwa shughuli tofauti mazingira yatakayosaidia
kuendelea kupata wahisani wengine wa ndani na nje nchi.
Moja ya malengo ya ushirikiano huo ni kusaidia jamii ya mji wa Masasi katika
kubadilishana teknolojia mbalimbali zenye uwezo wa kuleta tija kwa wananchi wa
mji wa Masasi ikiwemo matumizi sahihi ya majiko yanayotumia umeme jua pamoja na matumizi ya teknolojia ya
Bio gesi inayopunguza ukataji wa miti kwa ajili ya nishati ya kuni.
Ushirikiano huo pia umewezesha kwa baadhi ya
watendaji wa Halmashauri ya Mji Masasi kufanya ziara za mafunzo nchini
ujerumani kwenda kujifunza masuala mbalimbali ambapo hivi karibuni wanafunzi
wawili kutoka chuo cha maendeleo ya wananchi Masasi pamoja na walimu wao
walifanya ziara hiyo ya mafunzo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara akipokea hati ya makubaliano ya ushirikiano kutoka kwa mmoja wa wawakilishi wa wilaya ya Enzkreis kutoka nchini Ujerumani.
Mratibu wa ushirikiano kati ya Halmashauri ya Mji
wa Masasi na Halmashauri ya wilaya ya Enzkreis ya ujerumani Geofrey Martin
anasema kuwa wamekuwa na mahusiano mazuri na wilaya hiyo na kwamba hadi sasa
tayari baadhi ya miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Enzkreis imeshatekelezwa
kwa kiwango kikubwa huku mingine imeshakamilika.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa ufungaji wa mitambo ya Umeme jua katika
Hospitali ya Mkomaindo ambao umegharimu fedha za Kitanzania shilingi milioni 55 ambao
umesaidia kupunguza adha kubwa iliyokuwa ikijitokeza kutokana na kukatika kwa umeme mara kwa mara
ambapo pia kukamilika kwa mradi huo
kumesaidia kupunguza vifo vya akina mama waliokuwa wanashindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na watoto wanaozaliwa chini ya umri,ikiwa ni
pamoja na kupunguza gharama za kununua mafuta ya dizeli.
Martin anasema kabla ya ufungaji wa mitambo hiyo ya umeme
jua katika Hospitali ya Mkomaindo,Halmashauri ilikuwa inalazimika kutumia lita
400 za mafuta kwa ajili ya jenereta kwa mwezi zenye thamani ya shilingi 880,000
ambapo pia ilikuwa inalazimika kulilipa shirika la umeme TANESCO kiasi cha shilingi
milioni moja kwa mwezi mazingira yaliyopelekea kuifanya Halmashauri wakati
mwingine kutolipa kwa wakati madeni hayo.
Anasema maeneo yaliyopewa
kipaombele katika hospitali hiyo kwa awamu hii ya kwanza ya ufungaji wa mfumo
wa umeme jua ni pamoja na wodi ya wazazi na watoto,chumba cha maabara,chumba
cha upasuaji mkubwa na mdogo,chumba cha kupimia mionzi pamoja na chumba cha huduma ya baba, mama na
mtoto ili kukabiliana na vifo vya akinamama na watoto.
Kwa mujibu wa martin anasema
kuwa Enzkreis pia wamewesha kupatikana kwa Kifaa cha Kisasa cha Utra Sound katika Hospitali ya Mkomaindo hivyo kupunguza
adha kwa wananchi wa mji wa Masasi na vitongoji vyake ambao walikuwa
wanalazimika kutembelea umbali mrefu kwenda Hospitali ya misheni ya Ndanda
kufuata huduma hiyo.
Mratibu huyo anasema
katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi Halmashauri hiyo kutoka nchini
ujerumani tayari imeshafunga mitambo
ya Bio-gas katika Hostel ya Masista wa kanisa katoliki Migongo ambao awali walilazimika kuharibu
mazingira kwa kukata miti ili kupata kuni kwa ajili ya matumizi katuika hosteli
hiyo.
MRATIBU WA USHIRIKIANO HUO GEOFREY MARTIN AKIWA NA MMOJA WA WAWAKILISHI WA ENZKREIS.
Aidha anasema ufungaji wa
mfumo wa Bio-gas katika Chuo cha Maendeleo ya wananchi Masasi (FDC) umekamilika pamoja na
utengenezaji wa majiko ya jua chuoni
hapo haya yote yakiwa ni jitihada za Halmashauri katika kukabiliana na
uharibifu wa mazingira unaoathiri tabia nchi.
Anasema kuwa uongozi wa
chuo hicho cha maendeleo ya wananchi Masasi hapo awali ulilazimika kutumia fedha
zaidi ya shilingi milioni moja kwa mwezi kwa ajili ya ununuzi wa kuni ambao kwa
sasa umegeuka kuwa ndoto kwa uongozi wa chuo hicho.
Martin anasema ufungaji
huo wa mitambo ya Bio gesi umesaidia kupunguza gharama za uendeshaji katika
taasisi hizo ambazo kwa kiasi kikubwa hapo awali zililazimika kutumia kiasi
kikubwa cha fedha katika kupata kuni na kwamba uwepo wa teknolojia hiyo ya Bio
gas imechukua nafasi ya kuni,mkaa na mafuta ya taa na hivyo kusaidia katika
utunzaji wa Mazingira.
“Kimsingi miradi hii
imekuwa chachu ya maendeleo kwa Halmashauri pamoja na wananchi kwa ujumla…na
kwamba taarifa tulizonazo zinaonesha kuwa wananchi wengi wamekuwa wakiunga
mkono jitihada za Halmashauri kwa ushirikiano na Enzkreis zenye lengo la
kuufanya mji wa masasi kuwa mfano wa kuigwa”.Anasema Martin.
Mfumo wa umeme jua uliofungwa katika Hospitali ya Mkomaindo mjini Masasi kwa msaada wa Enzkreis.
Anasema miradi hiyo
imesaidia katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi katika utunzaji wa
mazingira ya mji wa Masasi kwa kuanzisha matumizi ya bio gesi ambayo hapo awali
hayakuwepo mazingira yaliyopelekea wakazi wengi wa mji huo kutumia nishati ya
kuni ambayo kwa namna moja ama nyingine huharibu mazingira.
Licha ya kuhifadhi
mazingira lakini pia wananchi wamepunguziwa gharama za maisha kwa kutumia kiasi
kidogo cha fedha kutoka kwenye maeneo wanayoishi ili kufika kwenye hospitali ya
mkomaindo tofauti na hapo awali ambapo wananchi walilazimika kutumia kiasi
kikubwa cha fedha kwa ajli ya kufuata huduma hizo muhimu.
Akisimulia namna
ushirikiano huo ulivyo muhimu kwa Halmashauri ya Mji wa Masasi,mratibu huyo
anasema kuwa hivi karibuni mnamo Agosti 6 mwaka jana hadi Agosti 16 wawakilishi
wa wilaya ya ya Enzkreis wakiongozwa na mratibu wao wa ushirikiano huo kutoka
wilaya hiyo Angela Gewiese aliyeongozana na Jana Edlinger walifanya ziara ya
ukaguzi wa miradi inayotekelezwa.
Anasema licha kukagua miradi hiyo inayotekelezwa wageni hao
walipata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo mengine na hivyo kuweza kuelezwa
baadhi ya changamoto ambazo kwa namna moja ma nyingine Enzkreis wameonesha nia ya kusaidia katika maeneo hayo
waliyotembelea.
Martin anasema miongoni
mwa maeneo yaliyotembelewa na yatakayonufaika na ushirikinao huo ni pamoja na
ufungaji wa taa za barabarani utakaoanzia
barabara ya Rest Camp kupitia
chuo cha Ukunga hadi hospitali ya Mkomaindo na baadye chuo cha wagnga
wasaidizi (COTC).
Aidha anasema upo
uwezeakano wa kuweka taa za barabarani katika eneo la makutano (Round about)
lililopo jirani na uwanja wa michezo wa boma mjini hapa zitakazosaidia kuepusha
ajali ambazo kwa sasa zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara kwa kukosa taa kwenye
eneo hilo hasa nyakati za usiku.
Anafafanua kwamba wilaya
hiyo ya nchini ujerumani iko tayari kutoa fedha kwa Halmashauri kwa ajili ya
ujenzi wa baadhi ya matundu ya vyoo katika shule ya msingi Nyasa na kwamba
Halmashauri imeagizwa kuandaa profoma
invoice ili waweze kutuma fedha mapema
kutokana na changamoto kubwa ya vyoo
waliyoiona katika shule hiyo.
Kadhalika ansema
Halmashauri inatarajia kupata fedha kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye
baadhi ya vifaa vya maabara katika hospitali ya Mkomaindo, ukarabati wa jiko la
Chuo cha Maendeleo ya wananchi
ambalo lipo katika hali mbaya pamoja na kuona uwezekano wa kutafuta
mahali ambapo patawekwa sanamu kama utambulisho wa ushirikiano wa Halmashauri
na Enzkreis.
“Nachukua fursa hii kutoa
mwito kwa watendaji wa Halmashauri wanaohusika kwenye maeneo ambayo
yanatarajiwa kupata msaada huo kuwa ni vyema wakaanza kushughulikia fursa hii kwa uaminifu na
uhakika mkubwa ili tusiwakatishe tamaa hawa wahisani wetu ambao wameonesha na
wanaendelea kuonesha nia ya kutusaidia katika Halmashauri yetu”. Anasema
Martin.
Anasema kuwa Enzkreis
wanao mpango wa kutoa msaada wa vifaa katika kituo cha Televisheni cha Masasi
kinachomilikiwa na Halmashauri ya mji wa Masasi ambacho kwa sasa kimeshindwa
kujiendesha kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kurushia matangazo.
Kadhalika anasema
Halmashauri ya mji wa Masasi kupitia kitengo chake cha habari na mawasiliano
kimekuwa kikifanya kazi katika wakati mgumu kutokana na kituo hicho kushindwa kurusha matangazo ya Biashara na ya
kijamii kutokana na tatizo la vifaa
kunakopelekea jamii ya Mji wa masasi na
vitongoji vyake kushindwa kupata habari
mbalimbali za ndani na nje ya nchi kwa wakati kupitia kituo cha Mtv.
Hata hivyo anasema kuwa licha
ya kuwepo kwa matatizo hayo ya vifaa katika kituo hicho cha Masasi
televisheni bado kituo kimendelea kutoa
matangazo yake kwa njia ambayo si nzuri na kwamba bado jitihada za kutafuta
wahisani waengine watakaosiadia kituo hicho zinaendelea.
Kwa mujibu wa mratibu huyo
anasema nia ya Enzkreis katika sekta hiyo ya habari na mawasiliano ni kuanzisha
kituo cha Redio kitakachokuwa na uwezo wa kurusha matangazo yake ndani ya mji
wa masasi na nje mazingira yatakayosiaidia jamii kupata habari juu ya namna
Halmashauri yao inavyotekeleza miradi mbalimbali kwa lengo la kutoa huduma
bora.
Eneo la Hospitali ya Mkomaindo Masasi
Anasema Halmashauri imepewa
kazi ya kuorodhesha vifaa vinavyotakiwa
katika uanzishwaji wa kituo cha redio na kwamba kazi hiyo tayari imeshafanyika kwa
ushirikiano na kitengo cha habari na mawasilinao na taarifa zimeshatumwa
kinachosubiriwa kwa sasa ni utekelezaji ambao unatarajiwa kuanza wakati wowote kutoka sasa.
Akizungumzia kuhusu sekta
ya michezo Martin ansema Enzkreis imekuwa kifanya jitihada kubwa ndani ya
Hlmashauri katika kuibua na kuendelea vipaji vya wanafuzni wa shule mbalimbali
pamoja na utoaji wa vifaa vya mihezo ikwemo mipira pamoja na jezi na kwamba
tayari wameaahidi kwa awamu hii watanunua
vifaa vya michezo katika timu yetu ya mpira ya Volley ball.
Kuhusu maktaba
anasema Halmashauri inayo maktaba ambayo
imekuwa ikifanya kazi kwa muda mrefu sasa ambapo katika kuboresha maktaba hiyo
jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika kama vile kutembelea shule za msingi,
sekondari pamoja na vyuo ili kuhamasisha
wanafunzi pamoja na kuomba misaada ya
fedha kutoka kwa wahisani wa ndani na nje ya nchi.
Aidha anasema ziko dalili za kuweza kusaidiwa katika Maktaba
yetu ya Mji wa Masasi ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa usafiri, ruzuku ya fedha kutoka
serikali kuu, upungufu wa watumishi wenye taaluma ya maktaba pamoja na uchakavu
wa jengo linalotumika kwa sasa ambapo zote kwa pamoja zinakwamisha utekelezaji
wa shughuli za maktaba hiyo.
Aidha changamoto nyingine inayoikabili maktaba ya
halmashauri ni upungufu wa vitabu vilivyo kwenye mtaala wa shule za msingi na
sekondari na kwamba kwa sasa ni vitabu
27 pekee ndivyo vilivyopo kwenye maktaba hiyo ambavyo viko kwenye mtaala wa
shule za msingi na sekondari wakati mahitaji ni Zaidi ya vitabu 3000.
Akizungumzia kuhusu mitambo ya mashine za kutengeneza
vipuri vya magari zilizoletwa kwenye chuo cha maendeleo ya wananchi Masasi
anasema Enzkreis tayari wameshaleta mashine hizo zitakazotumika katika
utengenezaji wa vipuri vya magari mazingira ambayo yatasaidia kuinua uchumi wa
chuo hicho.
MFANO WA TAA ZA BARABARANI AMBAZO ZINATAKIWA KUFUNGWA KWENYE BARABARA INAYOTOKA MKOMAINDO KUELEKEA CHUO CHA COTC.
Anasema pia wanafunzi wa chuo hicho pamoja na
walimu wao watapatiwa mafunzo ya utaalamu kutoka kwa wataalamu wa wilaya hiyo ya Enzkreis ya nchini ujerumani
juu ya namna ya utengenzezaji wa vipuri hivyo vya magari.
Martin anasema kufungwa kwa mashine hizo chuoni
hapo kutaisaidia vijana wa mji wa masasi kupata ajira chuoni hapo
zitakazosaidia kuinua maisha ya vijana hao ambao wengi wao kwa sasa hawana
ajira.
Kwa mujibu wa Martin alisema kuwa mitambo hiyo ni
imara na ya kisasa ambayo kama itatumiwa vizuri na wananchuo hao basi itakuwa
ni faida kwa wananchuo,walimu pamoja na jamii kwa ujumla kwani ni maeneo machache
hapa nchini yenye mashine kama hizo.
“Kama mashine hizi zitatumika kwa uangalifu na kwa
malengo yaliyowekwa basi ni dhahiri kuwa vijana wetu watapata ujuzi
utakaowasaidia huko waendako mara baada ya kumaliza mafunzo yao ya hapa chuoni
na kwamba hizo zote ni jitihada zetu zenye lengo la kuifanya Masasi iwe ni moja
ya miji yenye wataalamu wa fani mbalimbali”.Alisema Martin.
Mratibu huyo anasema wakazi wa mji wa Masasi
watumie fursa zilizopo kupitia mashine hizo za utengenezaji wa vipuri ili
waweze kujikwamua kiuchumi na kwamba ni vyema wakawapeleka watoto wao chuoni
hapo kwa lengo la kupata mafunzo hayo yatakayotolewa kwa ushirikiano na
Enzykreis.
Mashine zilizofungwa kwenye chumba cha X-RAY katika Hospitali ya Mkomaindo Halmashauri ya mji wa Masasi.
Anasema kuwa wao kama Halmashauri wako tayari
kutoa mafunzo kwa kushirikiana na idara ya maendeleo na ustawi wa jamii kwa
vikundi vya wanawake na vijana kwa gharama nafuu ili waweze kupata mafunzo ya
uundaji na utengenezaji wa vipuri vya magari pamoja na pikipiki.
“Vijana wajiunge kwenye vikundi walete maombi yao
kwa uongozi wa Halmashauri ya mji ili tuone ni kwa namna gani tunaweza
kuwasaidia katika kupata mafunzo hayo ya ujasiliamali ambayo kwetu ni moja ya
njia ya kupambana na umasikini kwa vijana na akinamama”.Alisema.
MFUMO WA UMEME JUA HOSPITALI YA MKOMAINDO MASASI
MWISHO
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD