TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Halmashauri ya mji wa
Masasi mkoani Mtwara imeendelea kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa
kidato cha nne kwa mwaka wa masomo wa 2014/2015 kwa kufaulisha kiwango cha
asimilia 48.78 kwa mwaka 2014 ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2013 ambapo
halmashauri ilifanikiwa kufaulisha kwa asilimia 32 kiwango cha ufaulu kikipanda kwa asilimia 16.68.
Pia ufaulu wa jumla
unaonesha kuwa wanafunzi 51 wavulana na
saba wasichana sawa na asilimia 14.15 wamefaulu kwa kupata alama za juu
zitakazowawezesha kujiunga na masomo ya kidato cha tano,vyuo vya ufundi pamoja
na vyuo vya ualimu.
Aidha taarifa hiyo
inaeleza kuwa wanafunzi wanne wavulana wamefanikiwa kufaulu kwa kiwango cha juu
huku waliofaulu kwa kiwango cha chini ni wavulana 81 na wasichana sita sawa na
asilimia 34.6 ambapo wanafunzi 192 wakishindwa kufaulu mtihani huo wakiwemo
wavulana 93 na wasichana 99 sawa na asilimia 47 ya waliofeli.
Akizungumza na gazeti
hili ofisini kwa niaba ya ofisa elimu sekondari Fatuma Msalazo kaimu ofisa
elimu sekondari wa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara Kangomba Saidi
alisema wanafunzi waliosajiliwa mwaka 2011 ni 415 wakiwemo wavulana 239 na
wasichana 176 huku waliofanikiwa kufanya
mtihani huo ni 410 sawa na asilimia 98.8 ya waliofanya mtihani wa kidato cha
nne kwa mwaka 2014.
Alisema Halmashauri
ya mji wa Masasi ina jumla ya shule za sekondari 10 ambapo kati ya hizo tisa ni
za serikali na moja ni ya binafsi na
shule zilizofanya mtihani ni tisa pekee huku shule ya sekondari ya wasichana ya
Masasi ikishindwa kufanya mtihani kutokana na wanafunzi wa shule hiyo kuishia
kidato cha tatu kufuatia serikali kusimamisha kwa muda wanafunzi wa kidato cha
nne na kuamua kuanzisha kidato cha tano na sita pekee.
Kwa mujibu wa
Kangomba alisema kati ya shule hizo tisa za Halmashauri ya Mji wa Masasi zilizofanya mtihani huo shule ya sekondari ya
Sululu kata ya Sululu imeongoza kwa
kushika nafasi ya kwanza kwa kupata wastani wa jumla wa asilimia 69 huku shule
ya sekondari ya Mwenge Mtapika ikishika nafasi ya pili ambapo nafasi ya tatu
ikishikwa na shule ya sekondari ya Mkuti mchanganyiko.
Kangomba alisema
matokeo hayo si miujiza kutoka kwa mungu bali ni umoja na mshikamano uliopo
miongoni wa wakuu wa idara,vitengo,idara ya elimu sekondari wakiongozwa na mkurugenzi
wao Fortunatus kagoro ambapo wamekuwa wakitumia muda mwingi kuhimiza masuala ya
elimu ya sekondari.
Alisema kushindwa kwa
baadhi ya wanafunzi kufanya mtuhani wa kidato cha nne mwaka 2014 kunatokana na
sababu mbalimbali zikiwemo mimba,utoro,vifo pamoja na mwitikio mdogo wa wazazi
wa kuwapeleka watoto wao shuleni.
Alisema kuwa ili kukabiliana
na changamoto hiyo idara ya elimu sekondari kwa kushirikiana na Halmashauri imeaandaa
mikakati kabambe ikiwa ni pamoja na shule zote kuanza kutoa huduma ya chakula
cha mchana shuleni,kuandaa kambi za mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na
mitihani,kuhimiza walimu kufundisha kwa bidii ikiwa ni pamoja na kutoa motisha
kwa walimu watakaofanya vizuri.
Aidha alisema kuwa licha
ya matokeo hayo mazuri lakini bado idara ya elimu sekondari inakabiliwa na
changamoto mbalimbali zikiwemo kuchelewa ama kutopatikana kabisa kwa fedha kutoka
serikali kuu za uendeshaji wa kazi za idara,ukosefu wa usafiri, pamoja na uhaba
wa vitendea kazi mazingira yanayosababisha idara kushindwa kufanya kazi kikamilifu.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD