TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Lugha ya kiingereza inayotumika katika uandaaji wa nyaraka
mbalimbali za mahakama za Wilaya pamoja na mahakama kuu nchini imekuwa ni
changamoto kubwa kwa wananchi wengi inayosababisha wananchi hao kushindwa
kuandaa nyaraka hizo na hatimaye kupoteza haki zao.
Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Masasi
mkoani Mtwara Asha Mwetindwa aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya siku
ya sheria nchini yaliyofanyika kwenye viwanja vya mahakama hiyo mjini humo.
Alisema wananchi wengi hushindwa kutumia fursa yao ya
kupata haki kutokana na kutoelewa lugha inayotumika katika sheria nyingi nchini
na kwamba wakati umefika kwa serikali wakishirikiana na wadau wa sheria kuona namna
ya kutumia lugha ya Kiswahili ili wananchi waweze kupata haki yao pindi
wanapokuwa na malalamiko.
Mwetindwa alisema dhana ya fursa ya kupata haki ni muhimu
na kwamba ni kipimo cha mfumo bora wa utoaji haki kwa jamii hivyo ni vyema
mihimili yote ya dola serikali,bunge na mahakama pamoja na wadau wa sekta ya
sheria wakatenda haki kikamilifu kwa mujibu wa sheria zilizowekwa.
Alisema uwepo wa taasisi huru za mahakama,mahakama
zinazofikiwa kwa urahisi,sheria bora na zilizowekwa kwa lugha inayoeleweka kwa
wananchi pamoja na uwepo wa wanasheria
wakujitegemea ni baadhi ya misingi ya fursa ya upatikanaji wa haki nchini.
Mwetindwa alisema serikali ina wajibu wa kuweka miundo
mbinu itakayorahisisha wananchi kuzifikia mahakama kirahisi na kwamba katika
kutekeleza wajibu huo Wizara ya katiba na sheria chini ya programu ya maboresho
ya sekta ya sheria inapaswa kuongeza kasi ya utoaji wa huduma za kisheria kwa
kuzingatia haki.
Aidha alizitaja changamoto zingine zinazoikabili idara ya
mahakama nchini ikiwemo gharama kubwa za ufunguaji kesi hasa za madai,uhaba wa
mawakili wa kujitegemea kwa sehemu zilizo pembezoni mwa nchi ikiwemo Wilaya ya
Masasi na Nanyumbu,umbali wa kuifikia mahakama pamoja na uhaba wa watumishi wa
mahakama.
Maadhimisho ya siku ya sheria nchini hufanyika kila mwaka
mwanzoni mwa mwezi februari ambapo maofisa waandamizi wa idara hiyo hupata
fursa ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kazi zinazofanywa na mahakama ambapo
kwa mwaka huu maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu ya dhana ya kupata haki,
wajibu wa serikali, mahakama na wadau.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD