TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Mtwara.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara
Halima Dendegu amewaagiza maofisa waandikishaji na wasaidizi wao kuhakikisha
kuwa wanatumia vyombo vya habari kufikisha ujumbe kwa wananchi katika zoezi la
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani humo.
Aidha amewataka kuacha
kufanya kazi kwa mazoea kwani kwa sasa tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia
kufanya mabadiliko makubwa katika uboreshaji wa daftari hilo kwa kutumia mfumo mpya ujulikanao kama Biometric Voters
Registration (BVR).
Aliyasema hayo jana
wakati wa ufunguzi wa semina iliyowahusisha waratibu wa Uandikishaji wa Mkoa,Ofisa Mwandikishaji, Maofisa
Waandikishaji Wasaidizi pamoja na maofisa wa Uchaguzi kwa ngazi ya wilaya na kata.
Alisema tume ya Taifa ya Uchaguzi ipo
katika maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia
teknolojia ya kisasa na kwamba mafunzo hayo yanalenga kuwapa uelewa jinsi ya
kutumia mfumo huo wa BVR.
Dendegu alisema BVR ni kifaa cha kisasa ambacho huandikisha
kwa kutumia kompyuta na kuchukua alama za vidole, saini na upigaji picha kwa
ubora wa hali ya juu ili kuondoa uwezekano wa wapiga Kura kujiandikisha zaidi
ya mara moja.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa Mkoa
alisema waandishi wa habari ni
wadau muhimu katika kufanikisha zoezi hilo hivyo ni vyema maofisa waliopewa
dhamana hiyo mkoani Mtwara wakatumia kikamilifu fursa hiyo ya habari katika
kuhamasisha na kuhabarisha wananchi waweze kujitokeza kujiandikisha.
“Ili wananchi waelewe
faida na umuhimu wa zoezi la daftari la kudumu la wapiga kura viongozi mliopo
hapa kwenye haya mafunzo ni lazima mtumie vyombo vya habari… vinginevyo zoezi
hili halitafanikiwa”.alisema.
Alisema mara nyingi
maofisa wanaopewa dhamana kwenye mazoezi muhimu kama hayo wamekuwa wakishindwa
kufikisha ujumbe kwa wananchi kutokana na kutoshirikiana na vyombo vya habari
mazingira ambayo husababisha vurugu zisizo na sababu na kwamba amewaasa hayo
yasitokee kwa mwaka huu.
Alisema anaamini kupitia
mafunzo hayo na kwa kutumia uzoefu walionao watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa,
kwa bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hilo la kitaifa na kwamba
wawe walimu kwa wenzao ambao hawajawahi kushiriki katika mafunzo hayo.
Aidha, Dendegu alieleza kuwa katika utaratibu wa sasa, kama ilivyokuwa
katika utaratibu wa zamani, wawakilishi wa Vyama vya Siasa wataruhusiwa kuwepo
katika vituo vya kuandikisha Wapiga Kura ingawa amewaonya kuwa hawatakiwi kuingilia
Watendaji wa zoezi hilo wanapotekeleza
majukumu yao.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini
iko kwenye maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa
kisasa utakaosaidia kuondoa kero na malalamiko yaliyokuwepo hapo awali ikiwa ni
pamoja na uwezekano wa mtu mmoja
kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD