TANGAZO
MKUU WA WILAYA YA MASASI FARIDA MGOMI |
Na Hamisi Nasri, Masasi
MKUU wa wilaya ya Masasi mkoani Mtwara Farida Mgomi ametoa wiki
mbili kwa watendaji wa kata na vijiji wakiwemo watendaji wa Halmashauri
zilizopo katika wilaya hiyo kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza wanaripoti shuleni vinginevyo hatua kali za kinidhamu
zitachukuliwa dhidi yao.
Mgomi alitoa wito huo juzi alipokuwa akizungumza na madiwani wa
Halmashauri ya mji wa Masasi pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Masasi kwa
nyakati tofauti kwenye vikao vya madiwani wa Halmashauri hizo.
Alisema idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza katika shule za sekondari wilayani Masasi bado hawajaripoti
shuleni hadi sasa jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa bado jamii haijazingatia
suala la elimu.
Alisema takribani asimilia zaidi ya 50 ya wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari wilayani
humo bado hawajaripoti shuleni hivyo watendaji wa kata waanze kuhamasisha
wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao aliofaulu wanakwenda shuleni.
Mgomi alisema hatokubali kuona watoto wamefaulu na wanashindwa
kuripoti shuleni bila ya sababu za msingi hivyo watendaji wa kata na vijiji
wanakila sababu ya kuhamasisha wazazi na walezi kuhakikisha wazazi wanawapeleka
shuleni watoto wao ili waweze kupata elimu.
“Idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha
kwanza wilayani hapa bado sasa hawajaripoti shuleni sasa natoa wiki mbili kwa
watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wazazi wanawapeleka watoto shuleni
vinginevyo nitachukua hatua kali,”alisema Mgomi
Aidha Mgomi aliwataka watendaji hao pia kuhamasisha kilimo
kwenye maeneo yao ili kuweza kuepeka wilaya kuomba chakula serikalini kila
mwaka na kudai kuwa iwapo wananchi wakitumia vema mvua zinazoendelea kunyesha
kwa kilimo tatizo la njaa litamalizika.
Alisema tatizo la njaa linasabishwa na wananchi kushindwa
kujikita katika kilimo hasa kwa kipindi hiki cha mvua hivyo kila mtendaji wa
kata na kijiji awajibike kwa nafasi yake kuhamasisha kilimo kwa wananchi.
Pia mkuu huyo wa wilaya alisema watendaji hao wa Halmashauri
wanapaswa kubadilika kiutendaji na kuanza kuona kuwa wanakila sababu ya
kuijenga wilaya ya Masasi kwa kushirikiana pamoja ili kuleta maendeleo chanya.
Alisema Halmashauri ya mji Masasi ndio kioo cha wilaya ya Masasi
hivyo watendaji hao wanapaswa kutambua kuwa bila kuwapo na msukumo wa pamoja
katika kuleta maendeleo na kwamba bila hivyo hadhi ya mji huo haitakuwapo.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD