TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Mkazi wa mtaa wa
Wapiwapi Halmashauri ya Mji wa Masasi mkoani Mtwara Kabura Joseph (35) ambaye
ni mfanyabiashara ya vinywaji amepigwa
risasi tatu, mbili chini ya titi lake la
kushoto na nyingine moja mgongoni na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi.
Tukio hilo la
kusikitisha limetokea juzi majira ya saa 2:30 usiku katika eneo la Wapiwapi
karibu na geti kuu la kuingilia nyumbani kwake wakati mfanyabiashara huyo
alipokuwa akirejea kutoka kwenye biashara zake.
Kamanda wa polisi
mkoa wa Mtwara Augustino Ollomi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema
kuwa majambazi hayo yalimvamia mfanyabiashara huyo na kufanikiwa kupora mkoba
wake ambao hadi sasa haijafahamika kuwa kulikuwa na vitu gani ndani ya mkoba
huo.
Alisema wakati
anarejea nyumbani usiku huo alikuwa na dereva wake wakiwa kwenye gari ndogo
isuzu Carrry iliyokuwa inatumika katika shughuli za usambazaji wa vinywaji kwa
wateja na kwamba walipofika nyumbani dereva alishuka kwenda kufungua geti ili
waingie ndani ya nyumba yao.
Kwa mujibu wa Kamanda
Ollomi alisema wakati dereva anafungua mlango wa geti hiyo,mfanyabiashara huyo
alishuka kwa lengo la kuhakikisha kama mlango wa gari yao uko salama kwa kuwa
ndani kulikuwa na vinywaji lakini mara baada ya kushuka ghafla alivamiwa na mtu
aliyemtaka atoe pesa na alipojibu kuwa hana ndipo alianza kumrushia risasi hizo
mazingira yaliyosababisha kupoteza fahamu.
Alisema polisi
walifika kwenye eneo la tukio na kumsaidia majeruhi huyo na kukimbizwa katika
hospitali ya misheni ya Ndanda kwa matibabu,ambapo madaktari wa hospitali hiyo
walifanikiwa kutoa risasi zote tatu kutoka kwenye mwili wa mfanyabiashara huyo.
Hata hivyo Kwa sasa
mfanyabiashara huyo jana jioni alihamishiwa katika Hospitali ya misheni ya
mtakatifu Walrburger Nyangao mkoani Lindi kwa matibabu zaidi.
Kufuatia kuongezeka
kwa matukio ya kihalifu wilayani Masasi jeshi la polisi limeanza kufanya
operesheni maalumu katika kuwasaka watuhumiwa wote wanaohusika ma matukio hayo
ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD