Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

WENYEVITI WA MITAA,VITONGOJI WATAKIWA KUACHA ITIKADI ZA KISIASA

TANGAZO
Hakimu Halfani Ulaya akiwaapisha viongozi hao
Waaswa kuacha itikadi za kisiasa
Na Clarence Chilumba, Masasi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi ambaye pia ni diwani wa kata ya Nyasa amewataka wenyeviti wa mitaa na vitongoji katika Halmashauri hiyo mkoani Mtwara kuacha mara moja itikadi zao za kisiasa ili waweze kutekekeleza majukumu yao kwa lengo la kuiletea Halmashauri maendeleo.

Aidha amewaagiza wenyeviti hao kusimamia usafi wa mazingira katika mji wa Masasi sambamba na kuhakikikisha kuwa watoto wote waliomaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2014 wanajiunga na kidato cha kwanza shule zitakapofunguliwa January 13 mwaka huu.

Pia amewaonya kutojiingiza kwenye migogoro isiyo ya lazima miongoni mwao na kwamba kuwepo kwa vitendo hivyo kwa viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza kama wao ni kusababisha wananchi kukata tamaa hivyo wakati mwingine kufanya maamuzi yasiyo na tija kwa jamii.

Aliyasema hayo jana wakati wa zoezi la kuwaapisha wenyeviti wa vitongoji na mitaa wa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani humo ambapo alisema itikadi zao za kisiasa zimeisha mara baada ya kuapa na kwamba kwa sasa kilichobaki ni kujenga uchumi wa Masasi kwa kushirikiana na wahisani wa nje pamoja na sekta binafsi.

Alisema Halmashauri ya Mji wa Masasi inategemea sana vyanzo vya mapato ya ndani ikiwemo kodi za majengo,maduka,leseni za biashara mbalimbali pamoja na ushuru wa mazao mchanganyiko na kwamba ili makusanyo yawe mazuri ni wajibu wa viongozi hao wa vitongoji na mitaa kutoa ushirikiano kwa maofisa wenye dhamana ya kukusanya mapato.

Mtumusha alisema kuwa pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Halmashauri  katika kusimamia usafi wananchi pia wana wajibu wa kutunza maeneo ya mji wa Masasi yasiharibiwe na kwamba hakusita kuwanyooshea kidole baadhi ya wananchi ambao wamekuwa na tabia ya kutupa takataka kwenye maeneo yaliyojengwa makalavati na mifereji hali inayopelekea kuziba kwa makalavati na mifereji hiyo  na kusababisha maji kuharibu barabara.
“Ndugu zangu wenyeviti wa mitaa na vitongoji kuongoza watu ni kazi inayohitaji moyo wa uzalendo na kwamba ili kufikia malengo mliyojiwekea ni lazima muwe wabunifu wa kubuni miradi ya maendeleo kwenye maeneo yenu… hapo mtakuwa mmetimiza majukumu yenu”.Alisema Mtumusha.
Akizungumzia kuhusu suala la uwepo wa viashiria vya vitendo vya rushwa kwa baadhi ya wenyeviti hao alisema ni wakati muafaka sasa umefika kwa viongozi hao kuacha vitendo hivyo na kwamba wazibe mianya yote ya rushwa inayoweza kujitokeza kwenye maeneo yao ya utawala.
Alisema viongozi hao wawe na moyo wa kujituma katika majukumu yao na kwamba watengeneze mbinu mbadala zitakazosaidia kuwahamasisha wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo ujenzi wa maabara unaoendelea mjini humo.
Mwisho.







TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top