TANGAZO
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya mji Masasi HENRY KAGOGORO. |
Wenyeviti wa vitongoji, vijiji na mitaa Masasi waapishwa.
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Jumla ya wajumbe 234
wakiwemo wenyeviti wa vitongoji 145, mitaa 58 pamoja na vijiji 31 wa
Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara wameapishwa rasmi huku wakiaswa kutenda
haki sawa kwa wananchi watakaowahudumia.
Aidha wameagizwa kufanya
vikao vya kisheria kwenye maeneo yao sambamba na kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi kwa kuwa
viongozi wengi wa ngazi hizo hawasomi taarifa hizo na kwamba atakayekiuka agizo
hilo atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Akizungumza wakati wa zoezi
la kuwaapisha wenyeviti hao kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi
mkoani humo Henry Kagogoro alisema wakati wa malumbano ya kisiasa umeisha na
kwamba kwa sasa kilichopo mbele yao ni kutimiza majukumu yao kwa wananchi
waliowachagua.
Alisema mara nyingi baadhi
ya viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi zao kwa mazoea huku baadhi yao
wakijihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya viongozi wa umma
kitu ambacho kwa awamu hii wamejipanga kukabiliana nacho.
Kagogoro alisema wanapaswa
kutoa ushirikiano kwa kwa uongozi wa Halmashauri na baraza la madiwani katika
kutekeleza majukumu yao ambapo pia wanapaswa kujua mipaka ya kazi zao ili
kuepuka migogoro isiyo ya lazima na watendaji wa Halmashauri hiyo.
Kwa mujibu wa kagogoro
alisema ni vyema wanapokuwa na kero mbalimbali ndani ya utendaji kazi wao
wakafuata taratibu, kanuni na sheria zilizopo huku wakionywa kuacha tabia ya
kujiona wao kuwa si sehemu ya uongozi wenye kutoa maamuzi na badala yake
kuiachia Halmashauri pekee mazingira yanayosababisha kero kwa wananchi.
Alisema uongozi ni kuonesha
njia kwa unaowaongoza hivyo ni jukumu lao kufanya hivyo katika kuwaletea
maendeleo wananchi wa Masasi pamoja na Halmashauri kwa ujumla na badala yake
waache tabia ya kulalamika kama wananchi kwani wao ni viongozi wanaopaswa
kuondoa malalamiko ya waliowachagua.
Katika utekelezaji wa
miradi mbalimbali ya maendeleo ya Halmashauri hiyo amewaagiza wenyeviti hao kuweka wazi mchakato wote wa
mradi unaotekelezwa sehemu husika na kwamba kukaa kimya kwao ndicho chanzo cha
vurugu na malumbano kwenye Halmashauri.
Akizungumzia kuhusu wajibu
wa jamii katika kutekeleza miradi ya maendeleo alisema jamii inayo jukumu la
kuonesha michango yao ha hali na mali katika kufanikisha miradi hiyo ikiwemo
ujenzi wa madarasa,nyumba za walimu,matundu ya vyoo,maabara na mabweni.
Alisema Halmashauri yake
imejipanga kutekeleza miradi yote ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kumalizia ile
ambayo haijakamilika hivyo aliwataka wenyeviti hao kuunga mkono jitihada hizo
za Halmashauri ili kuwaletea maendeleo wananchi wao.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD