Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

AJALI ZA BARABARANI MKOANI MTWARA ZAELEZWA KUPUNGUA KWA ASILIMIA 24

TANGAZO
Moja ya Ajali Mkoani Mtwara
Ajali za barabarani Mtwara zapungua
Na Clarence Chilumba, Mtwara

Ajali za barabarani  zinazozababishwa na vyombo vya moto vinavyotumia barabara katika mkoa wa Mtwara zimepungua kutoka ajali 177 mwaka 2013 hadi kufikia ajali 135 mwaka 2014 ambapo kati ya hizo ajali  71 zimesababisha vifo huku ajali 64 zikisababisha majeruhi.

Aidha kwa mwaka 2013 watu 336 walijeruhiwa huku mwaka 2014 watu waliojeruhiwa ni 190 pekee huku watu 95 wakipoteza maisha kwa mwaka 2013 na mwaka 2014 waliofariki dunia ni watu 85 na kwamba  ajali za pikipiki nazo zikiendelea kupungua kwa mwaka 2014 tofauti na mwaka 2013.

Pia ajali za pikipiki mkoani humo zimeendelea kupungua kwa kiwango kikubwa ambapo mwaka 2013 kulikuwa na ajali 77 huku mwaka 2014 zikiwa ajali 50 huku kati ya hizo 42 zikisababisha vifo kwa mwaka 2013 na kwa mwaka 2014 ni ajali 26 pekee ndizo zilizosababisha vifo.

Taarifa hiyo iliendelea kudai kuwa watu waliofariki katika ajali za pikipiki kwa mwaka 2013 ni 42 huku watu 27 wakijeruhiwa mwaka 2014 ambapo majeruhi wakiwa ni 83 mwaka 2013 na watu 62 wakijeruhiwa katika ajali mkoani humo kwa mwaka 2014.

Kamanda wa Polisi Mkoani Mtwara Augustino Ollomi aliyasema hayo wakati anaongea na mwandishi wa habari hii aliyetembelea ofisini kwake ili kupata taarifa za usalama barabarani kwa mwaka uliopita.

Alisema kwa ujumla kiwango cha ajali kimepungua kwa asilimia 24 mkoani humo kutokana na juhudi zinazofanywa na jeshi la polisi chini ya kikosi cha usalama barabarani na kwamba licha ya kiwango hicho kupungua bado jeshi la polisi mkoani Mtwara limejipanga kupunguza zaidi ajali hizo ambazo chanzo chake ni uzembe wa madereva.

“Licha ya kiwango cha ajali kupungua lakini bado takwimu hizi hazifurahishi hata kidogo… kwa kuwa bado maisha ya wananchi yanaendelea kupotea na wengine wakibaki na ulemavu wa kudumu na chanzo cha ajali hizi ni baadhi ya madereva ambao ni wazembe na wasiozingatia sheria kwa makusudi”.Alisema Ollomi.

Kamanda Ollomi alisema katika kupambana na madereva wazembe ambao huendesha vyombo hivyo vya barabarani bila kujali uhai wa watu wanaowaendesha jeshi lake mkoani humo limekuwa likiendesha operesheni maalumu ikiwemo zoezi la utozaji wa faini kwa madereva wanaokutwa na makosa mbalimbali wanapokuwa barabarani.

Alisema tayari wameshawafutia leseni madereva wanane kutokana na makosa mbalimbali huku jeshi hilo mkoani humo likifanikiwa kukusanya fedha kutokana na malipo ya faini jumla ya shilingi milioni 435 kwa mwaka 2014 huku mwak 2013 likikusanya kiasi cha milioni 305 ikiwa ni ongezeko la tozo la shilingi milioni 129.

Kwa mujibu wa kamanda huyo mkoani Mtwara alisema kwa mwaka 2013 jumla ya waendesha bodaboda 720 wamepitiwa kwenye vijiwe vyao vipatavyo 45 kwa ajili ya kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani na kwamba kutokana na elimu hiyo jumla ya waendesha bodaboda 1426 walipata leseni za udereva.

Kamanda Ollomi aliitaja mikakati iliyowekwa na jeshi hilo mkoani humo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa madereva,watembea kwa miguu pamoja na watumiaji wote wa barabara umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Aidha mikakati mingine iliyotajwa na kamanda Ollomi ni ukaguzi wa kila siku katika wilaya zote za mkoa wa Mtwara wa magari yanayoelekea jijini Dar es salaam ukaguzi ambao hufanywa na maofisa wa kikosi cha usalama  barabarani  ukaguzi wenye lengo la kupunguza ongezeko la ajali mkoani humo.

Kamanda huyo amewataka watumiaji wa barabara mkoani Mtwara kutii sheria za usalama barabarani bila shuruti kusudi kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika zinazochangia kupatikana kwa vifo, majeruhi,au vilema vya maisha.

Mwisho.





TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top