TANGAZO
KATIBU TAWALA WILAYA YA MASASI DANFORD PETER |
Na Clarence Chiumba, Masasi.
Wanawake hapa nchini wametakiwa kuipigia kura ya ndio katiba
inayopendekezwa ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea ya usawa wa kijinsia
maarufu 50:50 katika ushiriki wao kikamilifu katika nafasi mbalimbali za
maamuzi ikiwa ni pamoja na kupewa fursa ya kugombea nafasi za uongozi ndani ya
chama na serikali.
Aidha wameaswa kutoshawishiwa na baadhi ya wanasiasa
wanaombaza uvumi kuwa katiba hiyo inayopendekezwa haijazingatia mahitaji ya
msingi ya wanawake na kwamba wakifanya makosa katika katiba hiyo basi hata hayo
waliyoyakusudia hayatatekelezeka.
Pia wametakiwa kuachana na dhana iliyojengekea miongoni mwao
kuwa kila mara wamekuwa wakipewa vitisho na hata kukatishwa tamaa na wanaume kuwa
hawawezi kugombea nyadhifa mbalimbali ndani ya vyama na hata serikali na kwamba
wakati ukifika wajitokeze kugombea nafasi za uongozi.
Hayo yalisemwa jana na katibu tawala wa wilaya ya Masasi
mkoani Mtwara Danford Peter wakati anafungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea
uwezo viongozi wa jumuiya mbalimbali za vyama vya siasa yaliyoshirikisha
wajumbe wapatao 30 kutoka jumuiya za vyama vya CCM, Chadema, CUF pamoja na NLD
kutoka wilaya ya Masasi.
Mafunzo hayo yalifanyika kwenye ukumbi wa Umoja wa kanisa la
Anglikana Mjini Masasi ambayo yaliandaliwa na jumuiya za wanawake wa vyama
vyenye uwakilishi wa wabunge bungeni (ULINGO) yenye kauli mbiu isemayo “rafiki
wa mwanamke ni mwanamke na jirani wa mwanamke ni mwanaume”.
Katibu tawala huyo alisema wao wanapaswa kuwa wajumbe
wawakilishi wazuri kwa wanawake wenzao katika kueneza ujumbe wenye manufaa kwao
unaowataka kuipigia kura ya ndio katiba hiyo na kwamba mwelekeo wa katiba hiyo
hauwezi kueleweka bila ya wao wenyewe kujua haki zao za msingi zilizopo ndani
ya katiba inayopendekezwa.
“Wanawake viongozi wa jumuiya mbalimbali kutoka vyama vyenu
vya siasa mliopo hapa nawaasa muwe mabalozi wazuri kwa wenzenu waliopo nyuma
yenu…na kwamba kwa kuwepo kwenu hapa ni dalili tosha kuwa mmekubalika kwenye
jamii hivyo ni jukumu lenu sasa kutoa
elimu kwa wanawake wenzenu kuwa wakati ukifika waipigie kura ya ndio katiba
inayopendekezwa”.Alisema Danford.
Kwa mujibu wa katibu tawala huyo alisema kundi kubwa la
wanawake wamekuwa wakifanywa kama mtaji wa baadhi ya wanasiasa ambao huwatumia
pale wanapohitaji kuingia madarakani na kwamba amewataka kutokubali kuburuzwa
na badala yake waseme basi na wajitokeze wenyewe kwenye ushindani wa nafasi za
uongozi hapa nchini.
Kwa upande wake mjumbe wa sekretarieti ya Ulingo Saumu Rashidi
alisema si kweli kuwa wanawake hawajitokezi katika kugombea nafasi mbalimbali
bali wamekuwa wakipewa vitisho kutoka kwa wanaume na hata pale wanaposhinda
wamekuwa wakiambiwa kuwa waache nafasi hizo huku wakiahidiwa kupewa nafasi za
viti maalumu.
Alisema taasisi ya Ulingo kwa kushirikiana na TGNP,TAMWA pamoja
na LHRC wamejipanga kutoa mafunzo nchi nzima kwa vijana,wanawake na watu wenye
ulemavu yenye lengo la kuwajengea uwezo wa namna ya kuelezea sera ya vyama vyao
waweze kuchaguliwa katika maeneo yao.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD