TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Jumla ya vikundi vitatu vya
wanawake wajane wapatao 30 vilivyopo Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara
vimepatiwa fedha zaidi ya shilingi milioni 47 kutoka mfuko wa maendeleo ya
jamii Tasaf zitakazotumika kwenye programu maalumu ya uzoaji taka ngumu pamoja
na ufugaji wa nyuki.
Vikundi vilivyopatiwa fedha hizo ni
pamoja na kikundi cha Silabu kutoka kata ya Napupa, Nyasa B kutoka kata ya
Nyasa pamoja na kikundi cha wajane cha Magumuchila kata ya Mtandi vyote vikiwa
ni kutoka Halmashauri ya mji wa Masasi.
Pia katika kuhakikisha kuwa vikundi
hivyo vinafikia malengo yaliyokusudiwa Tasaf imetoa vitendea kazi vinavyohusika
na zoezi la uzoaji wa taka ikiwemo magari madogo yatakayorahisisha zoezi hilo
pamoja na mizinga ya nyuki kwa wale wa kikundi kinachotekeleza mradi huo wa
ufugaji nyuki.
Aidha vikundi hivyo vya wajane
vimeaswa kutambua kwamba fedha hiyo imeletwa kwa lengo maalumu na si kugawana
na kwamba fedha hizo walizopatiwa ni mtaji wenye lengo la kupunguza umaskini
kwa kujiongezea kipato miongoni mwao.
Akizungumza jana wakati wa ufunguzi
wa mafunzo ya kamati za usimamizi wa miradi ya Tasaf mwenyekiti wa Halmashauri
ya mji wa Masasi Andrew Mtumusha alisema lengo la mafunzo hayo ni kuzijengea
uwezo kamati hizo ili ziweze kutekeleza miradi yao vizuri na kwa uhakika kwa
kuzingatia taratibu za Tasaf.
Alisema kumekuwa na tabia sugu kwa
baadhi ya wanachama wa vikundi
mbalimbali vinavyopatiwa fedha za
maendeleo mjini Masasi kuacha kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na
badala yake waache ubabaishaji na wafanye shughuli za uzalishaji mali ili
waweze kujikomboa na janga la umaskini.
Mtumusha alisema wajane hao wana
wajibu wa kutekeleza mradi wa uzoaji wa taka ngumu pamoja na ule wa ufugaji wa nyuki
kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa na Tasaf na kwamba wawe mfano wa
kuigwa kwenye jamii inayowazunguka.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo
alisema Halmashauri ya mji wa Masasi kwa kushirikiana na serikali pamoja na
asasi zisizo za kiserikali imekuwa ikijitahidi kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa makundi mbalimbali ya
vijana,wazee na wanawake lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwa vikundi hivyo
kutumia fedha hizo kinyume na malengo yaliyokusudiwa.
Alisema wakati umefika kwa wananchi
mjini humo kuthamini sambamba na kuunga mkono jitihada zzinazofanywa na
Halmashauri yao na badala yake waache kuilaumu serikali kuwa haifanyi chochote
katika kuboresha maisha ya wananchi wake wakati kikwazo kikubwa cha maendeleo
ni wao wenyewe.
Naye mratibu wa Tasaf Halmashauri
ya mji wa Masasi Joram Msyangi alisema wameandaa mafunzo hayo ili kutoa maelekezo
ya awali juu ya majukumu ya kamati za miradi katika
usimamizi,ufuatiliaji,utoaji taarifa pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD