TANGAZO
Kikundi cha ujasiliamali cha KISIMA |
Mfumo dume unavyoathiri harakati za wanawake
Na Clarence Chilumba,
Masasi.
Vikundi mbalimbali vya
wanawake wajasiliamali wilayani Masasi vimelalamikia mfumo dume kutoka kwa
wanaume ambao wamekiri kuwa umekuwa ukirudisha nyuma jitihada zao za kujiletea
maendeleo yao mazingira yanayosababisha kuendelea kubaki kuwa tegemezi kwa
wanaume.
Pia wamelalamikia tabia
ya wanaume wengi kudhani kuwa kwa mwanamke kuwa na maendeleo basi ni kigezo cha
kumdharau mwanaume na hata kuvunja ndoa kutokana na kipato chake na kwamba
wamekuwa katika wakati mgumu na changamoto kubwa katika jamii inayowazunguka.
Aidha harakati zao za
kujikwamua kiuchumi zimekuwa kila mara zikikwamishwa kwa kuwekewa vikwazo na
wanaume ambao wamekuwa wakitumia ubabe mwingi kuzuia jitihada binafsi
zinazofanywa na wanawake hao wajasiliamali katika kujikwamua na janga la
umaskini ili waendelee kuwanyanyasa.
Kikundi hiko hufanya
shughuli mbalimbali zikiwemo utengenezaji wa sabuni ya maji, ufungaji na uuzaji
wa korosho, utengenezaji wa unga wa lishe pamoja na shughuli za mama lishe.
Akizungumza jana wakati
wa mahojiano na mwandishi wa Blog hii mwenyekiti wa kikundi sita Madeko (Kisima) kilichopo
eneo la Mkuti chini Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani humo Clara Myayaya
alisema si kweli kuwa wanawake hawataki kujishughulisha katika shughuli za
uzalishaji mali kama baadhi wa wanaume wanavyodhani bali wamekuwa wakikatishwa tamaa na hata
vitisho kutoka kwa wanandoa wao.
Alisema baadhi ya
wanachama katika kikundi hicho chenye wanachama 33 kwa nyakati tofauti wamewahi
kukumbwa na kadhia hiyo kutoka kwa waume zao ikiwa ni pamoja na kukatazwa
kushiriki kwenye vikundi hivyo vya ujasiliamali kwa madai kuwa wamekuwa
wakipoteza muda huku wengine wakidai vikundi hivyo vimekuwa vikijihusisha na
vitendo vya kihuni.
Kwa mujibu wa Myayaya
alisema kutokana na mfumo dume unaowanyima wanawake haki ya kushiriki kwenye
shughuli za ujasiliamali ndicho kinachosababisha wanawake wengi kuwa tegemezi
kwa kila kitu hata vile ambavyo wangeweza kujitafutia wenyewe.
“Wanawake si kama
hatuwezi kujitafutia ridhiki wenyewe tunaweza na ndio maana sisi tumeamua kuungana
pamoja na kuunda kikundi chetu cha ujasiliamali ambacho ni dhahiri kimekuwa na
mafanikio makubwa na tumeweza kubadilisha maisha yetu… ila ukweli ni kwamba
wanaume ni kikwazo kikubwa kwetu”.Alisema.
Akizungumzia kuhusu
mafanikio waliyoyapata kupitia kikundi hicho alisema wengi wao wamefanikiwa
kulipa ada za watoto wao, kujenga nyumba bora na za kisasa za kuishi pamoja na
kuwa na uwezo wa kujikimu kimaisha sambamba na kuboresha maisha yao ya kila
siku.
Myayaya alizitaja
changamoto zingine wanazokumbana nazo katika shughuli zao za kila siku ikiwa ni
pamoja na kukosa ofisi ya kufanyia kazi zao pamoja na kuuzia bidhaa zao,
ukosefu wa elimu ya ujasiliamali pamoja na mahudhurio duni ya baadhi ya
wananchama wa kikundi hicho.
Kikundi hicho cha Kisima
kilianzishwa Februari 2011 kikiwa kama ni kikundi cha kukopeshana maarufu
Vicoba ambacho kimeendelea kudumu na kukua hadi sasa na kwamba hadi leo
kimefanikiwa kuwa na akiba benki ya fedha zaidi ya shilingi milioni 16.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD