TANGAZO
Na Bashiru
Kauchumbe, Ruangwa.
Jumla ya
wanafunzi 830 kati ya 900 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa
mwaka wa masomo wa 2014/2015 katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi hadi sasa
hawajaripoti shuleni ikiwa tayari wiki moja imepita tangu shule hizo
kufunguliwa januari 13 mwaka huu.
Aidha taarifa
hiyo imedai kuwa hadi sasa ni wanafunzi 70 pekee ndio walioripoti shuleni licha
ya Halmashauri hiyo kuwa na idadi kubwa ya vyumba vya madarasa pamoja na walimu
kwenye shule zake za kata zilizojengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe.
Kufuatia
kusuasua kwa wanafunzi hao kutoripoti shuleni wadau wa maendeleo wilayani humo
wameanzisha kampeni ya kuhakikisha wanafunzi wote ambao wamechaguliwa kuingia
kidato cha kwanza katika shule mbalimbali kwa mwaka 2015 wanaripoti shuleni
haraka iwezekanavyo.
Hayo
yalibainika juzi wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya ya Ruangwa (DCC)
kilichofanyika kwenye ukumbi wa chama cha walimu (CWT) wilaya ya Ruangwa kilichoketi
kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo wilayani humo huku suala
la utoro wa wanafunzi hao likiwekwa kama azimio maalumu kwenye kikao hicho.
Wajumbe wa
mkutano huo walifikia maamuzi hayo magumu kufuatia
taarifa ya ofisa elimu sekondari wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Bihuria
Shabani iliyoeleza kuwa kati ya wanafunzi 900 waliochaguliwa kuingia kidato cha
kwanza kwa mwaka 2015 ni 70 tu ndio walioripoti shuleni hadi sasa.
Alisema hali ni mbaya na inasikitisha kuona wilaya ya Ruangwa
ikifaulisha wanafunzi wengi lakini cha ajabu hadi sasa wanafunzi wengi hawajaripoti
shuleni kwa uzembe wa wazazi na walezi wa watoto hao ambao wengi wao wamekuwa
wakifanya sherehe mbalimbali za kimila ikiwemo jando na unyago huku wakisahau
masuala ya msingi kwa wototo wao ikiwemo elimu.
Kwa mujibu wa Ofisa elimu huyo alisema baadhi ya wazazi
wilayani humo wamekuwa na utamaduni wa
kutowapeleka watoto wao kwa makusudi shuleni kwa kisingizio cha kutokuwa na
uwezo wakati kwenye shughuli za kijamii kama vile harusi wamekuwa wakitoa
zawadi na michango mikubwa na yenye thamani kubwa ya fedha na kwamba kwa mwaka
huu suala hilo kamwe halitakubalika.
“Wazazi wengi wilayani Ruangwa wamekuwa na tabia ya
kutowapelekea shuleni watoto wao wanapomaliza elimu yao ya msingi kwa
kisingizizo eti hawana uwezo… lakini cha ajabu wazazi hao wamekuwa wakijihusisha
na starehe mbalimbali zenye matumizi makubwa ya fedha ikiwemo unywaji wa pombe kama
vile kangara na gongo hakika hili kwa mwaka huu halikubaliki na kwamba tutakula
sahani moja na wazazi wote watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shuleni”.Alisema
Shabani.
Kwa upande wao wadau wa maendeleo wilayani humo wakiongozwa
na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo wameweka mikakati madhubuti itakayofanikisha
kampeni ya kuwasaka wazazi wote watakaosababisha watoto wao kutoripoti shuleni ikiwa
ni pamoja na wakuu wote wa shule hizo kuwapokea wanafunzi wote hata wale ambao
watakuwa hawajalipa ada pamoja na wale ambao watakuwa hawana sare za shule na
wazazi wapewe taarifa hizo.
Aidha mikakati mingine iliyowekwa na wadau hao ni kuendesha
zoezi la utambuzi kwa wanafunzi wote wa kidato cha kwanza waliochaguliwa kwa
mwaka huu zoezi litakalotumia askari mgambo wa vijiji na kata watakaoshirikiana
na maofisa watendaji wa kata na vijiji ili watoto wote waende shule mapema
iwezekanavyo.
Kwa upande wa kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na mkuu
wa wilaya ya Ruangwa Agnes Hokororo imepanga kufanya msako wa mtaa kwa mtaa,nyumba
hadi nyumba kuanzia februari 13 mwaka huu ili kuwabaini wazazi watakaoshindwa
kuwapeleka watoto wao shuleni na kwamba atakayebainika hatua kali zitachukuliwa
dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD