TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Mkazi wa kijiji cha Chinongwe Halmashauri ya wilaya ya
Ruangwa mkoani Lindi Juma Abdallah (40) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela
kwa kosa la kubaka kwa makusudi huku akijua kwa kufanya hivyo ni kinyume na
kifungu cha sheria namba 130.
Mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya
Masasi Asha Mwetindwa mwendesha mashtaka koplo Suleimani Omari alidai mshtakiwa
alitenda kosa hilo januari 1 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi huko katika
kijiji cha Liputu kilichoko Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Alidai kuwa mshtakiwa huyo alimbaka mtoto mwenye umri wa
miaka 13 (jina linahifadhiwa) mkazi wa Liputu wilayani humo na kumsababishia
maumivu makali kwenye baadhi ya viungo vyake.
Omari alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na
kwamba mshtakiwa ana kosa la kujibu na kuiomba mahakama imtie hatiani ikiwa ni
pamoja na kumpa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaotenda
vitendo hivyo vya kikatili kwa watoto.
Hakimu alimtaka mshtakiwa kutoa utetezi au kuuliza swali kwa
upande wa mashtaka lakini mshtakiwa huyo alidai kuwa hakuwa na swali lolote lile
la kuhoji zaidi ya kukiri kosa alilotenda.
Kwa upande wake mshtakiwa wa kesi hiyo Juma Abdallah alikiri
kosa ambapo alidai kuwa alitenda kosa hilo kutokana na ushawishi wa shetani na
kwamba hakujua madhara atakayoyapata mara baada ya kutenda kosa hilo na
aliiomba mahakama imwachie huru kwa kigezo kuwa ana majukumu mazito ya
kifamilia.
Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili hakimu mkazi
mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara Asha Mwetindwa
aliridhika na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka na kumtia hatiani
mshtakiwa huyo kwa kumpa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.
Aidha mshtakiwa huyo anatakiwa kulipa fedha shilingi milioni
moja kwa mtoto huyo aliyebakwa ikiwa kama fidia kwa kitendo cha kinyama
alichomfanyia kilichopelekea mtoto huyo kuhathirika kisaikolojia.
Habari zilizopatikana nje ya mahakama na kuthibitishwa na
jeshi la polisi wilayani Masasi zinasema kuwa mshtakiwa huyo kwa nyakati
tofauti mwaka jana amehusishwa kwenye matukio hayo ya ubakaji mara 12 ingawa
hakuwahi kutiwa mbaroni.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD