TANGAZO
Clarence
Chilumba,Ruangwa.
SHIRIKISHO la vyama vya
watu wenye ulemavu wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi (SHIVYAWATA) limeiomba serikali kuendesha oparesheni maalumu ya kutokomeza
vitendo vya mauaji dhidi ya walemavu wa ngozi (albino) ikiwa ni pamoja na
kuweka mikakati kwa ajili ya kuwabaini watu wanaojiusisha na matukio
hayo ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwito huo umetolewa
mwishoni mwa wiki na mwenyekiti wa shirikisho
hilo,Hamisi Jabiri wakati anazungumza na
mwandishi wa Blog hii ofisini kwake kuhusu mfululizo wa matukio ya kuuawa na
kukatwa viungo kwa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini ambapo alisema shirikisho
hilo wilayani Ruangwa limesikitishwa na mwendelezo wa matukio hayo
na kutaka uchunguzi wa kina ufanyike.
Alisema ikiwa serikali
inaweza kuendesha oparesheni tokomeza na kimbunga kwa ajili ya kudhibiti
ujangili wa kuuawa kwa tembo na rasilimali zingine hapa nchini inakuwaje ishindwe
kuwa na mikakati kabambe ya kuendesha
oparesheni ya kuwasaka watu wanaojihusisha na matukio ya kuuawa kwa walemavu wa
ngozi.
Jabiri alisema kuwa maisha
ya watu wenye ulemavu yako hatarini sana na kwamba hakuna jitihada zozote
zinazofanyika hivyo wameiomba serikali kuwawekea mazingira yaliyobora kiusalama
zaidi ili kudhibiti matukio ya kuuawa albino yasiendelee kutokea kwani
yanawafanya waishi kwa wasiwasi na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo kwa
amani.
Alisema iwapo serikali
ikielekeza nguvu zake kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuendesha oparesheni
maalumu nyumba hadi nyumba bila ya kujali gharama yoyote kwa ajili ya kuwasaka
watu wanaojihusisha na matukio hayo itasaidia kuwabaini wahusika wa vitendo
hivyo hatimaye kufikishwa katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo
wake.
“Mbona operasheni
kimbunga kuhusu ujangiri imefanyika kwa mafanikio kwanini serikali pia isifanye oparesheni
kuhusu matukio ya walemavu wa ngozi? Alihoji Jabiri.
Alisema ukosefu wa
chombo maalumu kinachoshughulikia changamoto za walemavu hapa nchini ni sababu
moja wapo ya kushindikana kwa udhibiti wa matukio hayo ya kukatwa viungo na
kuuawa kwa walemavu wa ngozi na kwamba serikali sasa inapaswa kutilia mkazo wa
kuanza kutafuta mwarobaini wa vitendo
hivyo.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti Moza Mchoya (16) na Agia Juma (41) ambao wote ni walemavu wa ngozi
katika kijiji cha Mtakuja kata ya Nanganga Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi walisema kuwa wamehawi
kusikia kupitia vyombo vya habari kwamba baadhi ya watu wenye ulemavu wa ngozi
kama wao wanauawa na kukatwa viungo vyao mazingira ambayo yaliwasababishia hofu
ya kuuawa kijijini hapo.
Waliendelea kueleza
kwamba imefikia hatua kwa wao kutoshiriki kwenye mikutano ya hadhara na
shughuli zingine za kijamii kijijini hapo hasa kwa zile zinazofanyika nyakati
za usiku kwa kuhofia kuuawa hivyo wameiomba serikali iwe macho kwa kuwa wao ni
watanzania ambao wanasathili kuthaminiwa kama walivyo wengine.
“Sisi tunaamini kuwa serikali haishindwi kitu
na kwamba inauwezo mkubwa wa kutokomeza
vitendo vya mauaji ya walemavu wa ngozi iwapo itathamini maisha ya kundi letu la watu wenye ulemavu wa ngozi kwa kuendesha
oparesheni maalumu dhidi ya mauaji hayo kama inavyoendesha oparesheni zingine
ikiwemo milipuko ya magonjwa kama vile dengue na sasa hivi ebola,kwa nini
ishindwe kwetu albino? Walimalizia…Mchoya na Agia.
Kwa upande wake diwani
wa kata ya Nanganga Shabani Kambona alisema jamii pia inapaswa kushiriki
kikamilifu katika kutoa taarifa kwa vyombo husika kwa ajili ya kuwasaka wanaohusika kwenye
matukio hayo ya kushambuliwa kwa walemavu wa ngozi nchini na kwamba ukiwepo
ushirikiano baina ya serikali, uongozi wa vijiji pamoja na jamii kwa ujumla vitendo hivyo vitatokomezwa
na kuwafanya walemavu hao kuanza kuishi kwa amani na kushiriki kwenye shughuli
za maendeleo.
Mwisho
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD