TANGAZO
Farida Mgomi mkuu wa wilaya ya Masasi |
Na Clarence Chilumba, Masasi
MKUU wa wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Farida
Mgomi ametoa onyo kali kwa viongozi wa vijiji vya Mwongozo,Mdenga pamoja na
Nangoo vilivyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani hapa iwapo
watashindwa kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu ambao
wanahujumu na kuharibu miundombinu katika mradi wa maji wa mamlaka ya maji safi
na Mazingira Masasi–Nachingwea (MANAWASA).
Mgomi ametoa onyo hilo mwishoni mwa wiki mjini
hapa baada ya mamlaka hiyo kutangaza rasmi kusudio la kusitisha huduma ya maji
kwenye vijiji hivyo vitatu kutokana na wananchi wake kuhujumu miundombinu ya
maji na kusababisha huduma hiyo muhimu kuzorota katika miji ya Masasi na
Nachingwea.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa mara kadhaa
amekuwa akipatiwa taarifa za uharibifu wa miundombinu ya maji kwenye maeneo ya
vijiji hivyo na kutoa maagizo kwa viongozi wa vijiji hivyo waweze kukaa kwa
pamoja na wananchi wao ili kuweka mikakati itakayosaidia kudhibiti na
kuwakamata watu wanaohusika kuharibu miuondombinu hiyo.
Mgomi alisema kuwa serikali imefanya jitihada
kubwa katika kuleta huduma ya maji kwa wananchi wa wilaya hizo ili kuweza
kusaidia kuondokana na tatizo la maji katika maeneo yao lilokuwa likiwakabili
kwa muda mrefu hivyo anashangazwa kuona wananchi wanashindwa kulinda rasilimali
hiyo muhimu na badala yake wanahujumu na kuharibu miundombinu hiyo.
Alieleza kuwa huduma ya maji ni muhimu kwa
binadamu ndio maana serikali imechukua hatua ya kuleta mradi huo ili kuwakomboa
wananchi wa Masasi juu ya tatizo la maji lakini kama viongozi na wananchi
watashindwa kulinda na kuthamini miuondombinu
na kuamua kuhujumu miundombinu lazima serikali iwachukulie hatua kali za
kisheria.
“Serikali imeleta mradi huu kwa ajili ya
kuwahudumia wananchi na kwamba viongozi wa vijiji tumewapa dhamana kusimamia na
kuulinda mradi kwa umakini mkubwa hivyo kama viongozi hawa wanashindwa kutimiza
majukumu yao juu ya mradi huu lazima niwachukulie hatua kali za kisheria”.alisema
Mgomi.
Aliongeza kuwa serikali kupitia uongozi wake wa
wilaya umeshafanya vikao mara kadhaa kwa wananchi na viongozi wa vijiji kuwahamasisha
wananchi juu ya umuhimu wa mradi huo mkubwa ambao unahudumia wakazi wa wilaya
ya Masasi na Nachingwea.
Mkuu huyo wa wilaya alisema watu wanaojihusisha
kuharibu miundombinu ya maji na kwamba wanalengo la kurudisha nyuma jitihada za
maendeleo katika wilaya hiyo na kwamba ni wazi wanapaswa kuchukuliwa hatua za
kisheria na serikali.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa mamlaka
hiyo ya maji Masasi–Nachingwea Manawasa, Nuntufye Mwamsojo alisema tayari uongozi
wake umeshakabidhi barua kwa viongozi wa vijiji hivyo ili kuwapa taarifa ya
kusudio la kusitisha huduma ya maji katika vijiji hivyo kutokana na wananchi
wake kuhujumu miundombinu ya maji.
Alisema hakuna sababu ya wao kuendelea
kuwapatia huduma ya maji katika maeneo hayo huku baadhi ya vifaa vya mradi huo
vinaharibiwa kila kukicha licha ya uongozi wa mamlaka hiyo kutoa agizo la
kulinda miundombinu ya maji.
Mwisho
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD