Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

TAASISI ZA FEDHA ZATAKIWA KUZITAMBUA HATI MILIKI ZA KIMILA KATIKA UTOAJI WA MIKOPO

TANGAZO
Ofisa Mawasiliano (Mkurabita) Gloria Mbilimonywa.
 Na Clarence Chilumba, Mtwara.
Halmashauri ya wilaya ya Mtwara ni miongoni mwa Halmashauri hapa nchini zilizonufaika na mpango wa kurasimisha rasilimali (Ardhi) na biashara za wanyonge Tanzania (MKURABITA) mpango uliotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2011/2012.

Katika utekelezaji wa mpango huo Halmashauri ilipokea zaidi ya shilingi milioni 47 lengo likiwa ni kuwapa nguvu za kiuchumi wananchi wa mkoa huo hasa wale wenye kipato cha chini kwa kuwaongezea uwezo wa kumiliki rasilimali walizonazo sambamba na kufanya biashara katika mfumo rasmi na wa kisasa zaidi wenye tija kiuchumi.

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kutokana na mpango wa Mkurabita ni pamoja na kuongeza usalama wa kumiliki ardhi miongoni mwa wananchi waishio vijijini,kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa kumiliki ardhi kisheria pamoja na kupatikana kwa hati miliki za kimila kwa wananchi hao.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa kurasimisha rasilimali ardhi kwa wilaya ya Mtwara jana mbele ya maofisa mawasiliano waliofanya ziara wilayani hapo ofisa ardhi wa Halmashauri hiyo Johnia Rwebangira alisema mpango huo ulianza novemba 2011 na kumalizika aprili 2012 na kwamba ili kufanikisha Halmashauri ilishirikiana na wataalamu kutoka ofisi ya Raisi.

Alisema upimaji wa mashamba uliofanyika kwa siku 21 uliwezesha kupimwa kwa kijiji cha Mkunwa na Shaba ambapo jumla ya wananchi wapatao 561 walipimiwa mashamba yao huku mashamba 600 yakipimwa na kuandaliwa sambamba na kusajiliwa katika daftari la usajili la hati miliki za kimila.

Rwebangira alisema kwa sasa mji wa Mtwara unakua kwa kasi kutokana na kuwepo kwa ongezeko kubwa ka watu linalotokana na ugunduzi wa gesi asilia mkoani humo na kwamba ni vyema wananchi wa mkoa wa Mtwara wakapima maeneo yao waweze kupata hati miliki za kimila.

Alisema licha ya kuwepo kwa mafanikio hayo ya mpango huo bado ziko changamoto kadhaa zinazoathiri mpango huo zikiwemo taasisi za fedha kutozipokea hati miliki za kimila kwa kuziona kuwa hazina hadhi sawa na zile zinazotolewa na kamishna wa ardhi pamoja na ukosefu wa fedha kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za urasimishaji ardhi ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kuweza kupata hati miliki za kimila.

Alizitaja changamoto zingine kuwa ni kugawanyika kwa vijiji mara kwa mara ambapo katika kipindi cha mwaka 2013/2014 Halmashauri ya wilaya ya Mtwara ilikuwa na jumla ya vijiji 157 na kata 28 na kwamba kwa sasa Halmashauri hiyo ina vijiji 206 na kata 38.

Kwa upande wake mtaalamu wa mawasiliano wa mpango wa urasimishaji rasilimali (Ardhi) vijijini (Mkurabita) Gloria Mbilimonywa alisema kuwepo kwa mpango huo hapa nchini kumesaidia kupunguza migogoro ya ardhi iliyokuwepo hapo awali na kwamba kwa sasa wananchi wengi wamehamasika kushiriki kwenye mpango huo wenye tija kwao.

Alisema serikali iendelee na jitihada za kuelimisha taasisi za fedha hapa nchini kuzipokea hati miliki za kimila ili kutimiza dhima ya kurasimisha rasilimali za wanyonge vijijini ili waweze kuingia kwenye mfumo rasmi wa kumiliki ardhi.

Mwisho.


Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Mtwara Johnia Rwebangira akiwaonesha hati miliki ya kimila maofisa mawasiliano serikalini (Hawako pichani) walipotembelea Halmashauri hiyo kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa mpango wa kurasimisha rasilimali (Ardhi) vijijini (MKURABITA).










TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top