TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Mtwara.
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa
kushirikiana na Serikali limeombwa kupeleka wataalamu wa kufanya tathmini na
kufahamu sababu za kumomonyoka kwa eneo ardhi kavu na kuwa sehemu ya bahari na
kutishia usalama wa kiwanda cha kuchakata gesi katika eneo la Msimbati mkoani
Mtwara.
Hayo yamezungumzwa jana na Meneja Mkuu wa
Kiwanda cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba mkoani humo, Leonce Mosso wakati wa
ziara ya Mkurugenzi wa Tanesco nchini, Felchesmi Mramba alipotembelea kiwanda
hicho.
Mosso alisema serikali ina kila sababu ya
kupeleka wataalamu kufanya tathmini kwani kitendo cha maji ya bahari kula
sehemu ya ardhi kavu linatishia usalama wa watumishi wanaoendelea na shughuli
zao.
Alifafanua kuwa, hali hiyo ilitokea usiku wa
kuamkia Januari 14 mwaka huu baada ya upepo mkali na mawingu
yaliyokuwa yakipiga kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kula eneo la ardhi kavu.
“Mvua ilisababisha eneo la ardhi kavu la zaidi
ya mita mia moja kuliwa na maji ya bahari ndani ya saa tatu na kubakiza mita 29
tu kufikia kilipo kiwanda hicho jambo ambalo linahatarisha miundombinu ya
kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo katika eneo hili,” alisema Mosso na
kufafanua kuwa;
“Endapo hali hiyo itaendelea iko hatari kwa
wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa gizani sambamba na kukwamisha mradi wa
usafirishaji wa gesi asilia kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kutokukamilika kwa
wakati.”
Hata hivyo, Mosso aliongeza kuwa, kufuatia uwepo
wa hali hiyo waliamua kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kuona
ni namna gani wanakabiliana na hatari ya kuharibika kwa miundombinu hiyo na
hivyo waliomba msaada kwa jeshi la wananchi ambapo wanajeshi wapatao 300
waliweza kujaza vifusi eneo maji yalipoishia ili kuzuia mmomonyoko usiendelee.
Aidha, Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika
hilo, Mramba alisema endapo hali hiyo ingeendelea ingepelekea mikoa ya Lindi na
Mtwara kukosa umeme kwani vyanzo vya umeme wanaotumia unatokea Msimbati.
Mramba alifafanua kuwa, kufuatia kitisho cha
mtambo huo wa Msimbati kuathiriwa na maji walikuwa tayari wamejiandaa kuhamisha
mtambo unaotumia mafuta wenye uwezo wa kuzalisha megawati 120 toka Dar es
Salaam kwenda Mtwara kukabiliana na hali hiyo lakini sasa uwezekano wa
miundombinu kuharibiwa umepungua.
Mtambo wa Msimbati kuna
kiwanda cha kuchakata gesi ambayo ndio inayotumika katika mikoa ya Lindi na
Mtwara na Madimba ndipo kinapojengwa kiwanda cha kuchakata gesi asilia ambayo
itasafirishwa kwenda Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD