TANGAZO
Na Clarence Chilumba, Mtwara.
Wafanyakazi
nchini wametakiwa kuzingatia misingi ya maadili katika utendaji wao wa kazi
sambamba na kufuata misingi ya utumishi wa umma iliyowekwa kwani wananchi ndio
wanaowategemea katika kuleta maendeleo ya Taifa.
Akizungumza
mkoani Mtwara jana wakati akifungua mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi wa
Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwa mwaka 2014/2015, Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi
Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika alisema imebainika kuwa kwasasa kumekuwa
na changamoto kubwa ya uzingatiaji wa maadili ya utumishi wa umma ikiwemo
kuwepo kwa vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya ofisi, pamoja
na vitendo vya rushwa.
“Ni
vyema baraza likasisitiza umuhimu wa watumishi kufanya kazi kwa
kufuata maadili na nidhamu ya hali ya
juu wakati wa kutekeleza kazi zao za ukaguzi bila kukubali kuyumbishwa,”
alisema Mkuchika.
Mkuchika
alifafanua kuwa, jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali, taasisi
zisizo za kiserikali na makundi mbalimbali katika jamii kuhusiana na
mapambano dhidi ya rushwa na kwamba rushwa inapotawala sehemu za kazi
husababisha madhara mengi kwa jamii.
“Naomba
kupitia baraza hili kusisitiza umuhimu wa watumishi kufanya kazi kwa maadili na
nidhamu ya hali ya juu, najua kuna changamoto kubwa sana mnazokumbana nazo
katika kutekeleza kazi zenu za ukaguzi muhimu ni kutokukubali kuyumbishwa daima
mfuate misingi na maadili katika utendaji kazi,” alisema Mkuchika.
Aidha,
Mkuchika aliongeza kuwa, changamoto nyingine inayowakumba wafanyakazi hao ni
kuwepo kwa uhaba wa majengo yao wenyewe kwa ajili ya ofisi hivyo kuwafanya
wapange na kwamba serikali bado inaendelea na jitihada za kuhakikisha kila
Halmashauri zinakuwa na ofisi zao.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali, Profesa Mussa Assad alisema bado wanakabiliwa na changamoto ya rasilimali
watu na kwamba ofisi inaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kupunguza suala
la kutegemea ofisi za wakaguliwa.
Assad aliongeza kuwa, jitihada zinafanyika za kujenga na kununua majengo kwa ajili ya ofisi kwa kutumia fedha za maendeleo za bajeti toka serikalini na fedha za miradi ya maendeleo.
“Pamoja
na hatua ya kuongeza watumishi lakini bado tuna changamoto ya rasilimali watu
hii ni kutokana na sababu mbalimbali, ukaguzi wa umoja wa mataifa ni kazi ngumu,
nyeti ambayo inahitaji wakaguzi wenye uelewa na umakini mkubwa kwenye mambo
yanayohusu ukaguzi na teknolojia ya kisasa, pamoja na serikali kuunda maeneo
mapya ya utawala kwa kuanzishwa mikoa mipya na Halmashauri, ” alisema Assad.
Uzingatiaji
wa maadili katika utendaji wa kazi wa wafanyakazi nchini pamoja na kufuata
misingi ya utumishi wa umma ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi pamoja na
kuleta maendeleo ya Taifa.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD