TANGAZO
Na Haika Kimaro, Mtwara.
Wadau wa maendeleo mkoani mtwara wameshauriwa
kushikamana ili kuleta mabadiliko mkoani humo ikiwa ni sambamba na kuchangia
fursa zilizopo na zinazoendelea kujitokeza mkoani humo.
Hayo yalisemwa juzi na katibu tawala mkoa wa Mtwara,Alfred
Luanda wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya 2015 iliyoandaliwa na
taasisi ya Entango zilizowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo ili kufahamiana
na kujenga mtandao mzuri.
Luanda alisema tangu kufika mkoani humo ni mara yake ya
kwanza kuona kitu kama hicho kinafanyika na kwamba aliwashauri wadau wote
kushirikiana ili kuleta mabadiliko zaidi mkoani humo.
“Tangu nije mkoani Mtwara ndio mara yangu ya kwanza kuona
kitu kama hiki kinafanyika kikubwa ni kuwa na ushirikiano na mshikamano zaidi
ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa zilizopo na zinazozidi kuja,nisingependa
kuona shughuli za hapa zikifanywa na watu kutoka nje”.Alisema.
Akizungumza kwenye hafla hiyo mkurugenzi wa Entango Emma
Kawawa alisema lengo la kufanya sherehe hiyo ni kuwakutanisha wadau mbalimbali
ili kuwawezesha kufahamiana na kutambuana kwa shughuli zao ili kuwawezesha
kushirikiana pale inapotakiwa.
Alisema kuwa sherehe hizo zimefanyika kwa mara ya kwanza
mkoani humo ikizingatiwa kuwa mkoa wa Mtwara ni mkoa ambao unaanza kukua
kiuchumi hivyo ni vyema wadau wa maendeleo kutambuana kwa lengo la kuwapa watu
nafasi ya kuchangamkia fursa zilizopo.
“Hii ni mara yetu ya kwanza kwa Entango kufanya kitu kama
hiki kikubwa ni kujenga mtandao (mawasiliano) ili watu waweze kufahamiana ili
hata pale zinapojitokeza fursa za kimaendeleo ambazo zitamsaidia hata yule mdau
wa kipato cha chini kuinua uchumi wake ajue anaanzia wapi”.Alisema Kawawa
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD