TANGAZO
MKURUGENZI WA MANAWASA NUNTUFYE .D. MWAMSOJO |
MANAWASA MBIONI KUSITISHA HUDUMA BAADHI YA VIJIJI
Na Hamisi .A. Nasri,Masasi.
MAMLAKA ya maji safi na usafi wa mazingira Masasi–Nachingwea (MANAWASA) imetangaza
rasmi kusitisha huduma ya maji kwa wakazi wa vijiji vya Mwongozo,Mdenga na
Nangoo vilivyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara kutokana na wakazi wa vijiji hivyo
kuhujumu miundombinu ya maji.
Aidha uongozi wa mamlaka hiyo umewaandikia barua maalumu
viongozi wa vijiji hivyo kwa ajili ya kuwapa taarifa ya kusudio la kusitisha
huduma ya maji katika vijiji hivyo ambapo vina jumla ya zaidi ya wakazi wapatao
6218 wanaonufaika na mradi huo.
Akizungumza mwishoni mwa
wiki katika mahojiano maalumu mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka hiyo Nuntufye
Mwamsojo alisema ni kwa muda mrefu sasa kumekuwa na tatizo kubwa la uharibifu
wa miundombinu ya maji unaofanywa kwa
makusudi na wakazi wa vijiji hivyo.
Alisema awali vijiji hivyo havikuwa na huduma ya uhakika ya maji
safi na kwamba mamlaka ya manawasa iliamua kupeleka huduma hiyo kwa wakazi
waishio katika vijiji hivyo ili kuondoa tatizo la ukosefu wa huduma ya maji.
Alisema katika hali ya kusikitisha wakazi hao wamekuwa
wakihujumu miundombinu ya mradi huo wa maji ikiwemo kuchimbua na kukata mabomba
ili kuchota maji bure kisha kuacha mabomba hayo yakimwaga maji muda wote hali
ambayo inasababisha kupungua kwa msukumo wa maji na hivyo kupunguza kasi ya
kujaa maji katika tanki kubwa linalopeleka maji wilayani Nachingwea.
Kwa mujibu wa Mwamsojo alisema vifaa vingine ambavyo vimekuwa
vikihujumiwa katika mradi huo ni pamoja na kuibwa kwa koki za mabomba ya maji
zilizopo katika viosk vya maji ikiwemo kiosk kilichopo katika kijiji cha
Mwongozo.
Alisema Mamlaka imekuwa ikifanya ukarabati wa miundombinu hiyo
mara kwa mara lakini hali hiyo ya uharibifu inayofanywa na wakazi hao imekuwa
ikiendelea kufanyika hatua ambayo kwa sasa mamlaka inajiandaa kusitisha huduma
ya maji kwa wakazi hao.
“Iwapo Kama hali hii itaendelea Manawasa inakusudia kuchukua
hatua ya kusitisha huduma ya maji katika maeneo hayo hii ni kutokana na vitendo
vya hujuma vinavyofanywa na wakazi wa vijiji hivyo ambapo kwa kweli
vinasababisha kukosekana kwa maji katika mji wa Masasi na Nachingwea”. Alisema.
Alisema ana matumaini makubwa kuwa viongozi wa vijiji hivyo
watalipa uzito suala hilo katika kuwasimamia wananchi hao ili wasiendelee
kuhujumu miundombinu hiyo ya maji na kukomesha kabisa vitendo vya aina hiyo
ambavyo havina msingi katika harakati za kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Masasi,Farida Mgomi alisema
kuwa mradi huo wa Manawasa unapaswa kulindwa
kwa pamoja na wananchi ambao wao ndio walengwa wakubwa katika
upatikanaji wa huduma ya maji safi na kuachana na vitendo vya hujuma.
Mgomi alisema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi wa
vijiji hivyo iwapo hujuma hizo zitaendelea kuwapo katika maeneo hayo kwani
serikali imefanya jitihada za kuwaletea wananchi huduma ya maji na kwamba kwa nini
wananchi wahujumu mradi huo ambao mlengwa ni wananchi mwenyewe huku viongozi
hao wakikaa kimya.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD