TANGAZO
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi. |
MADIWANI MASASI WAINGIA LAWAMANI
Na Clarence Chilumba,
Masasi.
Madiwani wa Halmashauri
ya wilaya ya Masasi wameingia lawamani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni tabia yao
ya vitisho kwa baadni ya watendaji wa Halmashauri hiyo mazingira yanayopelekea
watendaji hao kushindwa kufanya kazi zao kwa kujiamini.
Aidha baadhi yao
wametupiwa lawama za kuhusika kwenye biashara haramu za ununuzi wa korosho kwa
kutumia mfumo usio rasmi maarufu kangomba hivyo kusababisha Halmashauri hiyo
kukosa mapato yake ya ndani.
Malalamiko mengine yaliyoelekezwa
kwao ni kuingilia shughuli za kitaalamu zinazofanywa na watendaji hao kwa
kigezo kuwa endapo watakiuka matakwa ya madiwani hao basi wataazimiwa ikiwa ni
pamoja na kuhamishwa.
Akizungumza juzi wakati
wa kuapishwa kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji wa Halmashauri ya wilaya ya
Masasi mwenyekiti wa jimbo la Masasi wa chama cha Demokrasia na maendeleo
Chadema Musa Mwadewa alisema wanazo taarifa za kuaminika kuwa baadhi ya madiwani wa Halmashauri hiyo
kuhusika katika vitendo hivyo.
Alisema baadhi ya
madiwani wa Halmashauri hiyo wamekuwa na utamaduni wa kutoa vitisho kwa
watendaji ya kwamba wataazimiwa hata kama madai yao si ya msingi kwa maendeleo
ya Halmashauri hiyo.
Mwadewa alisema ni vyema
madiwani hao wakaacha tofauti zao na badala yake waungane pamoja ili kuiletea
maendeleo Halmashauri ya wilaya ya Masasi ili iwe mfano wa kuigwa.
Kwa mujibu wa Mwadewa
alisema vyama vya upinzani wilayani humo kazi yake kubwa ni kusimamia ya wananchi
na kwamba wananchi waondoe dhana ya kwamba vyama vya upinzani siku zote ni kikwazo
cha maendeleo ya wananchi.
Alisema wao wako tayari
kutoa ushirikiano kwa chama tawala pamoja na watendaji wa Halmashauri hiyo na
kwamba lengo la vyama vya upinzani ni kusukuma kwa kasi pamoja na kusimamia
miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Sisi tuko tayari
kushirikiana na watendaji wa Halmashauri hii endapo tu tutapewa ushirikiano ili
kuiwezesha Halmashauri hii ya Masasi kusonga mbele kimaendeleo”.Alisema
Mwadewa.
Alisema jeshi la polisi
pia wilayani humo limekuwa likibebeba lawama kwa kushindwa kutoa ushirikiano kwa
wananchi pale panapotokea matukio ya kihalifu na kwamba wananchi wanapotoa
taarifa hupewa majibu kuwa jeshi hilo halina mafuta ya kutosha kufika kwenye
tukio.
Alisema kushindwa kwa
jeshi la polisi katika kutoa huduma kwa wakati kwa wananchi pale wanapohitaji
ndicho kinachosababisha wananchi hao kuchukua sheria mikononi pale
wanapowakamata watuhumiwa wao.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD