TANGAZO
Baraza la madiwani Halmashauri ya wilaya Masasi |
Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji Watakaosababisha
njaa kukiona
Na Clarence Chilumba, Masasi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi ambaye pia ni diwani wa kata ya
Chiungutwa Juma Satma amewaagiza wenyeviti wa vijiji na vitongoji kusimamia kilimo kwenye maeneo yao na kwamba
atakayesababisha njaa katika eneo lake basi atakuwa hatoshi kubaki kwenye
nafasi hiyo.
Pia amewaagiza kutumia mamlaka waliyopewa
kisheria katika kudhibiti vijana wote wanaoshinda kwenye maeneo yasiyo rasmi
maarufu vijiwe ili kupambana na baa la njaa linaloweza kutokea endapo tu viongozi
hao watazembea.
Aidha wameonywa kuacha mara moja tabia ya
kufanya kazi kwa mazoea na badala yake watende haki kwa wananchi wote bila
kujali tofauti ya vyama vyao vya siasa
kwani jukumu lao ni kuwaletea maendeleo waliowachagua.
Kwa mujibu wa Satma alisema wananchi katika
maeneo walikotoka wanawategemea kuwaletea maendeleo na ndio maana wakawapa
dhamana ya kuwaongoza hivyo ni vyema wakawatumikia kikamilifu.
Alisema baadhi ya viongozi wa vijiji na
vitongoji wamekuwa na tabia ya ulevi wa kupindukia na kwamba kiongozi kama huyo
hafai kuachwa akiendelea na tabia hizo na kwamba wao ni mfano wa kuigwa kwenye
jamii hivyo ni vyema wakatenda yale yaliyo mazuri ili kurudisha imani kwa
waliowachagua.
“Wananchi waliowachagua wana imani, matarajio
pamoja na matumaini kwenu katika kutekeleza kazi zenu…ambapo kama mnavyojua
tupo kwenye msimu wa kilimo hivyo nawaagiza kila mtu kwa nafasi yake ahimize
suala la kilimo na kwamba atakayezembea atakuwa ameshindwa kutimiza haya
mliyoapa leo”.Alisema Satma.
Akizungumzia kuhusu suala la elimu alisema
Halmashauri ya wilaya ya Masasi kwa mwaka 2014 imeshindwa kufikia lengo
lililowekwa na mkoa wa Mtwara la kila wilaya kufaulisha kwa kiwango cha
asilimia 55 ambapo alisema jukumu lao la kwanza kwa viongozi hao ni kuhakikisha
wanafanya vizuri kwenye mtihani wa mwaka huu.
Alisema kwa mwaka huu Halmashauri hiyo imeweka
mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza tatizo la wanafunzi wengi
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kutoripoti shuleni ikiwemo
kuwafikisha mahakamani wazazi wote watakasababisha watoto wao kutoripoti
shuleni.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD