TANGAZO
MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA RUANGWA MKOANI LINDI ISSA LIBABA
NA CLARENCE CHILUMBA,RUANGWA.
Abiria zaidi ya 100 waliokuwa wakisafiri kutoka
wilayani Ruangwa kuelekea Dar es salaam na mikoa ya Lindi na Mtwara
walilazimika kusitisha safari zao kwa takribani siku mbili mfululizo kusubiri
kuondolewa kwa lori lililokwama katikati ya mlima wa Namburuputwa kata ya Nkowe
Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Lori lililokwama kwenye eneo hilo ni aina ya scania
lenye namba za usajili T 324 BVE mali ya Frank Traders Limited ambalo lilikuwa
limebeba shehena ya mbolea zaidi ya mifuko 660 aina ya minjingu iiyoletwa miaka
mitatu iliyopita wilayani humo na kuhifadhiwa kwenye ghala la chama cha msingi
Likunja Amcoss.
Aidha uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa
shehena ya mbolea hiyo iliyoletwa wilayani humo zaidi ya miaka mitatu iliyopita
ilikuwa inarejeshwa jijini Dar es salaam baada ya wakulima wilayani Ruangwa
kutohitaji mbolea hiyo na kwamba kabla ya shehena hiyo tayari mifuko 640
ilisharudishwa mwishoni mwa wiki iliyopita huku tani kadhaa zikiwa bado
zimesalia kwenye ghala la Likunja.
Kufuatia kuharibika vibaya kwa barabara hiyo itokayo
Nanganga kuelekea Ruangwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha wamiliki wa
mabasi wametumia mwanya huo kupandisha nauli kutoka shilingi 5000 ya awali hadi
kufikia shilingi 7000 kutoka Nanganga kuelekea Ruangwa.
Maeneo yaliyoharibika ni yale katika vijiji vya
Michenga, Chimbila, Namahema, Mpumbe, Nkowe pamoja na Kitandi vyote vikiwa ni
kutoka wilaya ya Ruangwa mazingira yaliyopelekea abiria kutembea kwa miguu huku
wengine wakilazimika kubadilisha magari zaidi ya moja.
Katika hatua nyingine hoja hiyo ya ubovu wa barabara
wilayani Ruangwa iliibuka kwenye kikao cha baraza la madiwani la Halmashauri
hiyo kilichoketi jana kwa ajii ya kupitia na kupitisha bajeti katika mwaka wa
fedha wa 2015-2016 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Rutesco wilayani humo.
Akizungumza kwenye kikao hicho makamu mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ambaye pia ni diwani wa kata ya Nambilanje
Mosa Mtejela alisema hali ni mbaya kwani ziko baadhi ya barabara muhimu
wilayani humo ambazo kwa sasa hazipitiki kabisa na kwamba wakazi wa maeneo hayo
walilazimika kutembea kwa umbali mrefu kwa miguu.
Alizitaja barabara hizo kuwa ni pamoja na ile ya
Ruangwa-Mbekenyera-Namichiga hadi Nambilanje ambapo barabara zingine ni pamoja
na ile inayotoka Namichiga kuelekea Nambilanje ambayo juzi haikupitika kabisa
huku magari zaidi ya 15 yakikwama.
Alisema kwa sasa wananchi wa maeneo hayo wanalazimika
kusafiri kwa kutumia usafiri wa pikipiki ambao hapo awali nauli kutoka Ruangwa
mjini kuelekea Mbekenyera ilikuwa shilingi 15,000 na kwamba kwa sasa imepaa
hadi kufikia shilingi 40,000 kitu ambacho amekiri ni mzigo mkubwa kwa wananchi
waishio kwenye maeneo hayo.
Kwa upande wake meneja wa wakala wa barabara (TANROAD)
mkoa wa lindi Eng; Mwanawima alipotakiwa kutoa maelezo ni hatua gani
wanazichukua kufuatia malalamiko hayo ya madiwani wilayani Ruangwa alisema
hayuko tayari kuzungumza chochote kwa wakati huo na badala yake atafutwe kesho
aweze kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD